Serikali ya Marekani imesaini makubaliano ya ushirikiano na Tanzania katika masuala ya kuimarisha jeshi, ulinzi wa amani na usalama wa nchi dhidi ya maadui.
Ushirikiano huo uliosainiwa kupitia Programu ya Ushirikiano na Vikosi vya Majimbo vya Ulinzi wa Taifa, pia utahusisha kubadilishana uzoefu katika uchumi, kilimo, afya na kijamii.
Taarifa iliyotolewa katika ukurasa wa Instagram wa Ubalozi wa Marekani Tanzania, imeeleza ushirikiano huo unalenga kuimarisha uwezo wa taasisi na wataalamu wa pande zote, huku ukichochea maendeleo ya jamii na usalama wa wananchi.
Mkataba huo wa ushirikiano umetiwa saini na Meja Jenerali Craig Strong, Kiongozi Mkuu wa Walinzi wa Taifa wa Jimbo la Nebraska na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ), Jenerali Jacob Mkunda, mbele ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho.
Makubaliano hayo yanaimarisha zaidi mahusiano ya kimkakati kati ya Tanzania na Marekani, huku yakilenga kuongeza uwezo wa JWTZ katika kulinda amani, usalama na mipaka ya Tanzania dhidi ya vitisho vyovyote.








