Friday, December 12, 2025
spot_img
HomeMichezoMashabiki warahishiwa safari ya Morocco kuishangilia Taifa Stars AFCON 2025

Mashabiki warahishiwa safari ya Morocco kuishangilia Taifa Stars AFCON 2025

By Shufaa Lyimo

Mashabiki wa soka nchini wamepatiwa unafuu wa usafiri kuelekea Morocco kuishangilia timu ya taifa, Taifa Stars, inayotarajiwa kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) zinazoanza Desemba 21 mwaka huu. Hatua hiyo imeratibiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Baraza la Michezo la Taifa (BMT) pamoja na kampuni ya usafirishaji ya Blueberry Travels.

Akizungumza kwa niaba ya BMT, Benson Chacha alisema mpango huo umeanzishwa baada ya mashabiki wengi kupiga simu na kutuma ujumbe kuulizia namna ya kusafiri kwa pamoja kwenda Morocco.

“Kumekuwa na mwitikio mkubwa wa mashabiki kutaka kujua jinsi ya kusafiri. Ndiyo maana BMT na TFF tukatafuta kampuni itakayorahisisha safari, na tumepata Blueberry Travels ili kuwawezesha mashabiki wengi kwenda kuipa sapoti Taifa Stars,” alisema Chacha.

Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Blueberry Travels, Kelvin Charles, aliishukuru TFF na BMT kwa kuwapa nafasi hiyo, akibainisha kuwa wameandaa vifurushi rafiki kwa kuzingatia vipato vya Watanzania. Vifurushi hivyo vinajumuisha nauli ya kwenda na kurudi, malazi na usafiri wa ndani nchini Morocco.

Kwa mujibu wa Charles, gharama za vifurushi ni kama ifuatavyo:

  • Mchezo wa Tanzania vs Nigeria (Desemba 21):
    • Mtu mmoja: $2,535
    • Wawili: $2,320 kwa mtu
  • Mchezo wa Tanzania vs Uganda (Desemba 27):
    • Mtu mmoja: $2,970
    • Wawili: $2,700 kwa mtu
  • Mchezo wa Tanzania vs Tunisia (Desemba 30):
    • Mtu mmoja: $3,000
    • Wawili: $2,780 kwa mtu
  • Kifurushi cha michezo yote:
    • Wawili: $4,400 kwa mtu
    • Mtu mmoja: $5,250

Kwa upande wa maandalizi ya timu, Ofisa Habari wa TFF, Cliford Mario Ndimbo, amesema kikosi kinaendelea vizuri na maandalizi, huku morali ya wachezaji ikiwa juu.

“Wachezaji waliokuwa nje ya nchi wanaendelea kuripoti kambini kujiunga na wenzao. Malengo makubwa ni kufika hatua ya mtoano, ambayo itatupa nafasi nzuri ya kusonga hadi robo fainali,” amesema Ndimbo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments