Mashindano Baiskeli Shinyanga sasa yanukia kuwa ya kimataifa 


BAADA ya kufanyika kwa mafanikio kwa misimu mitano sasa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, ameishauri Benki ya CRDB kuyapandisha hadhi mashindano ya Baiskeli Shinyanga kuwa ya kimataifa.

Macha alitoa ushauri huo kwenye mashindano ya mbio hizo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki yakijumuisha wakimbiaji kutoka mikoa yote ya Kanda ya Ziwa na maeneo mengine nchini.

“Mbio hizi za baiskeli ni utambulisho wa mkoa wetu kwani leo taifa zima linatambua kuna jambo linaendelea hapa Shinyanga. Nafurahi kuona idadi kubwa ya wananchi mmejitokeza kushiriki, hivyo kupata nafasi ya kufahamiana na kujumuika pamoja kwa furaha. Ninachowaomba waandaaji ambao ni Benki ya CRDB, wakaribisheni washiriki kutoka nje ya mipaka ya Tanzania. Nafahamu mnatoa huduma Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), waleteni waendesha baiskeli kutoka huko waje tushindane nao. 

“Shinyanga tupo tayari kushindanishwa na yeyote yule, hivyo hata kama mtaona kuna waendesha baiskeli katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, wakaribisheni waje tuoneshane umwamba. Naamini kabisa, zawadi zote wataziacha hapa na wataenda kusimulia walichokiona Shinyanga,” alisema mkuu huyo wa mkoa.

Licha ya washindi kupewa zawadi, mbio hizo zilitanguliwa na uchangiaji wa damu ambapo zaidi ya chupa 500 zilipatikana suala ambalo Kaimu Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Benki ya CRDB, Anselm Mwenda, aliwashukuru wafanyakazi wenzake pamoja na wananchi wote walioshiriki kuchangia akisema zitakuwa na manufaa makubwa kwa wagonjwa wenye uhitaji. 

“Zaidi ya chupa 507 za damu salama zilizokusanywa si haba, zitasaidia kukidhi mahitaji kwa baadhi ya wagonjwa. Napenda kutumia fursa hii pia kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kuchangia damu kwani hujui itamsaidia nani kuokoa maisha yake. Kila siku tunasikia ajali na wagonjwa wakikimbizwa hospitalini, miongoni mwao wapo waliopungukiwa damu hivyo tujitahidi kujitoa kwa ajili yao,” alisema Mwenda akibainisha kuwa mwaka huu kimepatikana kiasi kingi zaidi ikilinganishwa na misimu iliyopita.

Kuhusu wito wa kuyafanya Mashindano ya Baiskeli Shinyanga kuwa ya kimataifa, Mwenda alisema watalifanyia kazi kwa kuwasiliana na mamlaka husika kuona waanzie wapi kuwapata washiriki kutoka mataifa ya Afrika Mashariki.

“Tumeupokea ushauri wa mheshimiwa mkuu wa mkoa. Tutaufanyia kazi ndani, kisha tutazishirikisha mamlaka husika kuona namna ya kuileta jamii ya Afrika Mashariki hapa Shinyanga. Ni jambo linalowezekana, naamini mwakani mashindano haya yanaweza kuwa na sura ya kimataifa,” alisema Mwenda.

Katika mashindano hayo, wanaume walikimbia umbali wa kilomita 150 na washindi walikuwa Boniface Ngwata kutoka Mwanza, Masunga Duba wa Simiyu na Frank Emmanuel kutoka jijini Dar es Salaam. Katika kundi hili, mshindi wa kwanza alijinyakulia Sh. milioni 1.5, wa pili aliondoka na Sh. 800,000 na wa tatu alijinyakulia Sh. 400,000. 

Kundi la pili lilikuwa la wakimbiaji chipukizi waliokimbia kilomita 80 ambalo Frank George wa Shinyanga aliongoza akifuatiwa na Joseph Paschal na Emmanuel George wote wa Shinyanga. Washindi hawa waliondoka na Sh. 800,000 kwa mshindi wa kwanza huku wa pili akizawadiwa Sh. 600,000 na wa tatu Sh. 300,000.

Kundi la mwisho lilikuwa la wanawake ambao walishindana kukamilisha mizunguko 20 katika uwanja wa mpira na zawadi zao zilikuwa Sh. 500,000 kwa mshindi wa kwanza, Sh. 300,000 na Sh. 200,000 kwa msindi wa pili na wa tatu. Kundi hili liliongozwa na Makirikiri Joseph wa Shinyanga alikifuatiwa na Florah Samwel wa Dar es Salaam na Sindano Makirikiri wa Shinyanga pia. Mshindi wa nne katika makundi yote aliondoka na Sh. 100,000 na wale walioshika nafasi ya tano mpaka ya 10 walizawadiwa Sh. 50,000 kila mmoja. 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *