Kylian Mbappé, mshambuliaji wa Real Madrid, ameweka wazi hisia zake baada ya kukosa penalti muhimu dhidi ya Athletic Bilbao mapema mwezi huu, akisema anajua anaweza kutoa mchango mkubwa zaidi kwa timu yake.

Mbappé alifunga bao lake la 14 msimu huu katika ushindi wa 4-2 dhidi ya Sevilla, akiimarisha rekodi yake ya mabao sita katika LaLiga. Hata hivyo, amekosolewa kwa kushindwa kutekeleza penalti mbili muhimu, dhidi ya Liverpool kwenye Ligi ya Mabingwa na Athletic Bilbao katika LaLiga.
“Naweza kufanya mengi zaidi,” Mbappé aliambia Real Madrid TV. “Ninajua nina uwezo mkubwa, na kila siku natamani kuonyesha uwezo wangu kwa jezi ya Madrid.”
Licha ya changamoto, Mbappé tayari ameshinda mataji mawili akiwa na Madrid, ikiwa ni UEFA Super Cup na Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia, akifunga katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Pachuca nchini Qatar.
Mbappé alisema kuwa anajisikia vizuri zaidi sasa baada ya kumaliza kipindi cha marekebisho na kuelewana zaidi na wachezaji wenzake. Madrid wapo katika nafasi nzuri kwenye LaLiga, wakiwa pointi moja nyuma ya Atletico Madrid na pointi mbili mbele ya Barcelona, kuelekea mapumziko ya Krismasi.