Mbunge aliomba Bunge liipe meno NEMC

Mbunge wa Sumve mkoani Mwanza, Kasalali Mageni, amesema kuna haja ya kufanya marekebisho ya sheria haraka ili kulifanya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwa mamlaka.

Mbunge huyo ameyasema hayo  bungeni mkoani Dodoma wakati akichangia hotuba ya makadirio ya bajeti ya  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuph Masauni.

 Hotuba hiyo  ya mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/2025 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/2026 iliwasilishwa bungeni.

Amesema NEMC kama chombo chenye dhamana ya mazingira nchini kinatakiwa kusimamia mazingira kwa misingi ya Sheria na kutoa maamuzi yasiyoingiliwa wala kupingwa na mtu yeyote.

“Tukizungumzia suala la kelele, wananchi wamekuwa wakiteseka, baa zimejaa kila kona, bila kujali vibali vya maeneo husika, NEMC wakifungia, mamlaka nyingine zinakuja zinafungua, kwa hiyo inakuwa ni ngumu kusimamia utekelezaji wake wa maagizo yake,” amesema

Amesema mazingira yanaendelea kuharibiwa na shughuli za kibinadamu kutokana na kukosekana kwa mamlaka yenye nguvu ya kuchukua hatua kwa wanaoendelea kuharibu mazingira.

Awali,  akiwasilisha hotuba ya mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/205 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/2026 Mhandisi Hamad Masauni, amesema Baraza litaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, sura 191 kwa kuendelea kutekeleza sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021.

Kadhalika, Waziri alisema NEMC  itaendelea kutekeleza mkakati wa Taifa wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), kuendelea kuratibu mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira, kusajili wataalam elekezi wa Mazingira na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya hifadhi na usimamizi wa mazingira.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *