Friday, December 19, 2025
spot_img
HomeHabariMbunge Kibiti aahidi kusimamia Ilani ya CCM na kuharakisha maendeleo ya wananchi

Mbunge Kibiti aahidi kusimamia Ilani ya CCM na kuharakisha maendeleo ya wananchi

Mbunge wa Jimbo la Kibiti mkoani Pwani, Amina Mussa Mkumba, ameahidi kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuhakikisha wakazi wa jimbo hilo wananufaika na maendeleo endelevu.

Amina ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha ziara yake ya kwanza ya kutembelea taasisi za serikali na binafsi wilayani humo, tangu alipoapishwa kuwa Mbunge.

Amesema ziara hiyo imelenga kujitambulisha pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo yanayohitaji kufanyiwa kazi, hususan yale aliyoyapata kutoka kwa wananchi wakati wa kampeni.

“Hii ni ziara yangu ya kwanza tangu kuapishwa. Nimeamua kutembelea ofisi za serikali na binafsi ili kuzungumza masuala yatakayowezesha wilaya yetu kupiga hatua za maendeleo, hasa yale niliyoyaahidi wananchi wakati wa kampeni,” amesema Amina.

Katika ziara hiyo, Mbunge huyo amesema alitembelea Ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na kujadili umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira.

Ameeleza kuwa baadhi ya vijana wamekuwa wakilalamikia kuchukuliwa kwa bidhaa walizotengeneza kwa kutumia mbao, lakini baada ya mazungumzo na TFS ilibainika kuwa elimu kwa jamii inahitajika ili kuondoa migogoro hiyo.

Amesema TFS iko tayari kutoa elimu kwa jamii kuhusu utunzaji wa miti, madhara ya ukataji holela wa misitu pamoja na njia sahihi za uvunaji wa miti, ikiwamo kuanzisha misitu ya vijiji itakayowanufaisha wananchi.

Amina amesema Wilaya ya Kibiti ina maeneo yenye ukame, hivyo elimu ya upandaji wa miti inayostahimili ukame ni muhimu, sambamba na kunufaika kiuchumi kupitia ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa asali.

Aidha, amesema katika ziara hiyo alitembelea Ofisi za TANESCO na kufanya mazungumzo na Meneja wa shirika hilo, ambaye amemuahidi kuwa vijiji na vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na umeme vitapatiwa huduma hiyo ifikapo Januari mwakani.

Ameeleza kuwa Wilaya ya Kibiti ina jumla ya vijiji 56, ambapo vijiji 52 tayari vina umeme, huku juhudi zikiendelea kuhakikisha vijiji vilivyosalia vinaunganishwa.

Mbunge huyo amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuwaletea wananchi maendeleo, akieleza kuwa kupitia nguzo za zege aina ya “delta”, huduma ya umeme sasa imefika maeneo mengi zaidi.

Akizungumzia mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na makundi maalum, Amina amesema amejiandaa kuhakikisha makundi hayo yananufaika ipasavyo na mikopo ya halmashauri.

Amesema mikopo hiyo ilianza kutolewa katika awamu iliyopita lakini ilikumbwa na changamoto zilizolazimu kusimamishwa, kabla ya kurejeshwa tena na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, huku kiwango cha fedha kikiongezwa.

Ameeleza kuwa tayari matangazo yametolewa na makundi 23 yamenufaika na mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 200.

Amina amesema pamoja na kuwepo kwa vigezo vya kupata mikopo, halmashauri ina wajibu wa kuwaelekeza wale wasiokidhi vigezo ili waweze kujiandaa na kunufaika katika awamu zijazo.

Ametoa wito kwa wananchi wanaokosa vigezo kutochoka wala kukaa kimya, bali kutoa taarifa ili kusaidiwa, huku akiwataka wanufaika wa mikopo kuitumia kwa uzalishaji, kuongeza kipato na kurejesha kwa wakati ili kujenga uaminifu.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments