Mfanyakazi wa Benki ya NMB, Lilian Mandali (31), amefariki dunia baada ya kuzama katika maporomoko ya maji yaliyopo Hifadhi ya Mpanga Kipengere, mkoani Njombe, alipokuwa akijaribu kuwaokoa watoto wawili waliokuwa wakizama. Watoto hao, Michelle Mwasongwe (5) na Jannel Mwasongwe (4), nao walipoteza maisha katika tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amethibitisha kutokea kwa mkasa huo, akieleza kuwa ulitokea Septemba 14, 2025 majira ya saa nane na nusu mchana, wakati wa sherehe ya pamoja (get together) ya wafanyakazi wa NMB kutoka matawi ya Makambako, Wangingโombe na Makete.
Taarifa zinaeleza kuwa watoto hao, ambao ni wa Bertha Nicodem, mfanyakazi wa NMB tawi la Makambako, walijitosa kuogelea katika maporomoko hayo kabla ya kushindwa kuyamudu maji. Lilian Mandali alijitosa majini kuwasaidia, lakini naye alizama na kupoteza maisha.
Miili ya marehemu imeopolewa na kuhifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Mbuyuni, wilayani Mbarali.




