Na Mwandishi Wetu, Pwani
Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani linamshikilia Ally Shabani (29), mganga wa tiba asili na mkazi wa Makazi Mapya, Mlandizi wilayani Kibaha, kwa tuhuma za mauaji ya Juma Nyambihira.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Muhudhwari Msuya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), alisema tukio hilo lilifichuka baada ya ndugu wa marehemu kutoa taarifa ya kupotea kwake tangu Agosti 17. Taarifa hizo zilikabidhiwa Kituo cha Polisi Mlandizi mnamo Agosti 29, mwaka huu.
Kwa mujibu wa ACP Msuya, baada ya taarifa hizo polisi walifungua jalada la uchunguzi na kuanza kufuatilia. Hatua hiyo ilimfikisha mikononi mwao mtuhumiwa Shabani, ambaye inadaiwa alikuwa akiishi na marehemu Juma akimpatia matibabu ya asili kutokana na tatizo la uoni hafifu.
Mwili Wapatikana Katika Shimo
Kamanda Msuya alieleza kuwa mnamo Septemba 3, wakati upelelezi ukiendelea, askari walifika nyumbani alipokuwa akiishi mtuhumiwa pamoja na marehemu kwa ajili ya upekuzi. Katika eneo hilo, walibaini uwepo wa tanuri la mkaa lililokuwa karibu na nyumba hiyo, ambapo kando yake kulionekana dalili za shimo.
“Baada ya kufukuliwa, tulibaini ndani ya shimo hilo ulikuwa mwili wa marehemu Juma Nyambihira,” alisema ACP Msuya.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi.
Mtuhumiwa Kufikishwa Mahakamani
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa mtuhumiwa Ally Shabani atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika, huku likiendelea na hatua za uchunguzi ili kubaini undani wa tukio hilo.




