Saturday, December 13, 2025
spot_img
HomeHabariMgombea urais NLD aahidi hospitali ya kisasa Kiteto na kudhibiti migogoro ya...

Mgombea urais NLD aahidi hospitali ya kisasa Kiteto na kudhibiti migogoro ya ardhi

Mgombea Urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, ameahidi kujenga hospitali ya kisasa katika vijiji vya Kijungu na Pori kwa Pori vilivyopo Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara endapo atachaguliwa, ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wakazi wa maeneo hayo.

Akihutubia wananchi leo, Septemba 14, 2025, Doyo alisema wakazi wa vijiji hivyo hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, ama Kiteto Mjini au Songe wilayani Kilindi, jambo linalohatarisha maisha yao hasa katika dharura.

“Nafahamu mnakabiliwa na changamoto nyingi, lakini changamoto ya afya inabeba msingi muhimu katika ujenzi wa taifa. Ili tujenge taifa imara tunahitaji wananchi wenye uhakika wa huduma za afya. Hospitali ya kisasa hapa itapunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu,” alisema Doyo.

Katika mkutano wake mwingine na wananchi wa Kiteto Mjini, Doyo aligusia changamoto ya migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, akibainisha kuwa baadhi ya taarifa zinazotolewa na wananchi zimekuwa zikikosa ukweli na kuibua tuhuma zisizo sahihi dhidi ya viongozi.

“Wakati mwingine wananchi wanapotoa taarifa wanakuwa waongo na kuwatuhumu viongozi bila ushahidi. Nikichaguliwa Rais, nitahakikisha tunahamisha na kuleta upya sekretarieti ya Kiteto ili kupima kwa usahihi taarifa zenu na kuhakikisha tunapata ukweli,” alieleza.

Aidha, ameeleza kuwa serikali yake itawaweka askari wa wanyamapori katika maeneo ya makazi ya watu ili kudhibiti tembo wanaovamia mashamba na kusababisha madhara kwa wananchi. Pia ameahidi kuunda tume maalum ya kutengeneza ramani itakayoweka mipaka ya wazi kati ya maeneo ya wakulima na wafugaji, ili kudhibiti migogoro ya mara kwa mara.

Doyo alisisitiza kuwa serikali yake haitavumilia kundi lolote litakalokiuka makubaliano ya vikao vya kimila au ya serikali, huku akiahidi kuwa wananchi waliopata hasara kutokana na uvamizi wa tembo watapewa fidia stahiki kama kifuta jasho.

Baada ya kumaliza ziara yake Kiteto, msafara wa kampeni wa Doyo umeelekea Wilaya ya Babati kuendelea na mikutano ya hadhara.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments