Monday, March 9, 2026
spot_img
HomeHabariMjumbe Maalum wa UN aipongeza Tanzania kurejesha amani kuimarisha taasisi za kidemokrasia

Mjumbe Maalum wa UN aipongeza Tanzania kurejesha amani kuimarisha taasisi za kidemokrasia

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika (UNOAU), Parfait Onanga-Anyanga, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua ilizochukua kurejesha amani na utulivu kufuatia vurugu na matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea katika baadhi ya maeneo ya nchi Oktoba 29, 2025.

Onanga-Anyanga, ambaye ni Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres, alitoa pongezi hizo alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya mwanzo wa mazungumzo yake na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa kitaifa.

Mjumbe huyo yupo nchini kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kufanya mashauriano na Serikali na wadau wengine wa kitaifa kuhusu hali ya kisiasa nchini, pamoja na kujadili namna Umoja wa Mataifa unavyoweza kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kusimamia mageuzi na kuendeleza umoja na mshikamano wa kitaifa kupitia maridhiano jumuishi.

Aidha, amempongeza Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha utulivu na uongozi makini katika kipindi kigumu kilicholikabili taifa. Pia amepongeza uamuzi wa Serikali wa kuunda Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Onanga-Anyanga pia aliipongeza Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, akieleza kuwa ina ubora na weledi wa hali ya juu unaokidhi viwango vya kimataifa. Alisema muundo wa tume hiyo unaojumuisha wajumbe kutoka kada mbalimbali umeongeza uhuru na ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha, ameipongeza Serikali kwa juhudi za kurejesha imani ya wananchi na kudumisha utulivu baada ya matukio hayo, pamoja na hekima iliyotumika katika kushughulikia changamoto zilizojitokeza wakati wa kipindi cha uchaguzi.

Katika muktadha huo, Mwakilishi huyo Maalum ameukaribisha mpango mpana wa kitaifa uliotangazwa Januari 2026 chini ya kaulimbiu ya “Repair – Rebuild – Renew,” akisema kuwa mpango huo unaweka msingi muhimu wa kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kusimamia mageuzi ya taasisi pamoja na kuendeleza maridhiano ya kitaifa.

Vilevile, amempongeza Waziri Kombo kwa juhudi zake za kuielezea jumuiya ya kimataifa hatua na michakato ya ndani ya nchi inayochukuliwa kushughulikia matukio hayo na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Katika ratiba ya ziara yake nchini, Onanga-Anyanga anatarajiwa kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ACT Wazalendo, Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya utawala bora, demokrasia na mshikamano wa kitaifa.

Aidha, anatarajiwa kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge, Jaji Mkuu pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni wawakilishi wa mihimili mitatu ya dola.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje, Mahmoud Kombo ameishukuru Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano wake na kueleza kuwa Tanzania inathamini sana ushirikiano huo. Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na UN na haitasita kuomba msaada pale inapohitajika katika kuimarisha taasisi za taifa na kulinda amani, utulivu na mshikamano wa wananchi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments