Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan ameahidi kuutazama Mkoa wa Arusha kwa jicho la kipekee, ili kuendelea kuwa mkoa wa kimkakati.
Amesema Arusha ni mkoa wa kimkakati unaohitaji miundombinu ya kutosha ili kukuza utalii, amefafanua kuwa mikoa mingine inaanza sasa, lakini Arusha na Zanzibar ndio maeneo ya utalii Tanzania.
Dkt Samia ameeleza hayo Ijumaa Oktoba 3,2025 wakati akizungumza na wananchi wa majimbo ya Karatu, Ngorongoro na Monduli katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mnadani wilayani Karatu.
Mkutano huo ulikuwa wa mwisho kwa mujibu wa ratiba Dkt Samia za Mkoa wa Arusha, ambaye baadaye ataelekea mkoani Manyara.
“Arusha ni mkoa wa kidiplomasia, taasisi nyingi za kimataifa zipo hapa. Arusha ni mkoa wa wakulima na wafugaji, ni mkoa wa kimkakati unaohitaji jicho la pekee,”
“Ahadi yangu lile jicho la pekee, tutajitahidi kulilete ili Arusha ubakie mkoa wa kimkakati,” ameeleza Dkt Samia.
Aisifu Arusha, asema ukanda kaskazini unakuwa kijani
Mgombea huyo, hakuacha kuwasifu wagombea na viongozi wa CCM mkoani Arusha kwa namna walivyojipanga kuelekea uchaguzi wa Oktoba 29, akisema tangu awasili mkoani humo ameshuhudia maandalizi mazuri.
“Kila aliyesimama hapa (wagombea ubunge na viongozi CCM) amesema kura kura zitapigwa hivi huku kwingine zitapigwa vile.Niwapongeze sana, hii itakuja kuleta heshima ya ukanda wa kaskazini,”
“Huko nyumba ukanda wa kaskazini haukuwa ukitizamwa kwa jicho la chama tawala, lakini kwa namna toka nilivyoingia Arusha, ninavyosikia wagombea wanayoyasema, viongozi wa kimila na ahadi zao, maeneo mengi wamekuja na majani kwamba mama yaliyopita yamepita tutazame mbele, nawashukuru sana,” amesema Dkt Samia.
Katika maelezo yake, Dkt Samia amewahidi wananchi wa Ngorongoro, Monduli na Karatu ujenzi wa Barabara mbalimbali za majimbo hayo ili kurahisisha shughuli za kijamii ikiwemo utalii.
“Tutaendelea na usambazaji wa kilimo, ujenzi wa mabwabwa ya kilimo.Yule mkandarasi aliyesuasua kujenga bwawa la Eyasi, ameshaondolewa anatafutwa mwingine ili kuendelea na ujenzi huo.
“Tutajenga soko maeneo ya Kona tarafa ya Eyasi, tutanunua mashine nne za boti za uvuvi na kuboresha mwalo katika ziwa Eyasi ili kutengeneza ajira kwa vijana,” ameeleza.
Kuhusu mifugo, Dkt Samia amesema Ilani ya CCM imepanga kuongeza maeneo ya wafugaji kutoka ekari milioni 3.6 hadi milioni 6, sambamba na kuwafundisha wafugaji kuhusu ufugaji wa kisasa, na upandaji wa nyasi na kuepeka kuzunguka kusaka malisho.
“Tutakwenda kukarabati miundombinu ya minada ya mifugo na kujenga majosho 13 na machinjio ya kisasa,” amesema Dkt Samia.
Pia, Dkt Samia amelichukua ombi la uwekaji wa taa katika barabarani kuanzia Mto wa Mbu, Karatu hadi lango la kuingia hifadhi ya Ngorongoro amelichuka.




