Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dodoma, Dkt. Fredrick Sagamiko, ameeleza kuwa ujio wa Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) umekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto mbalimbali zinazolikabili jiji hilo.

Akizungumza katika mahojiano maalum, kiongozi huyo alibainisha kuwa moja ya miundombinu inayoendelea kujengwa ni barabara zenye urefu wa kilomita 10.19. Barabara hizo zitawawezesha wananchi kufika maeneo ya huduma mbalimbali kwa urahisi, kupunguza gharama za usafiri na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa.
Aidha, Dk. Sagamiko alieleza kuwa kupitia mradi huo tayari ujenzi wa Soko la Majengo unaendelea. Alifafanua kuwa hapo awali wafanyabiashara walifanya shughuli zao katika mazingira magumu, lakini sasa mradi huo utawapatia soko la kisasa lenye huduma mbalimbali ikiwemo maegesho ya magari. Pia, idadi ya wafanyabiashara itaongezeka na kufikia jumla ya watu 875.
“Ujio wa mradi huu katika jiji letu ni ukombozi tosha kwa wananchi, maana hali ya Soko la Majengo ilikuwa haiendani na hadhi ya Dodoma. Lakini sasa tunaelekea kupata soko jipya,” amesema Dk. Sagamiko.




Kuhusu maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huo, Dk. Sagamiko alibainisha kuwa yapo maendeleo ya ujenzi wa mitaro ya maji katika eneo la Ilazo, ujenzi wa stendi ya daladala katika eneo la Nzuguni pamoja na mnada mpya. Alisisitiza kuwa eneo la Nzuguni lina idadi kubwa ya watu, hivyo uwepo wa stendi ya daladala ni hitaji muhimu.
Kwa upande wake, Rozy Mtundu, ambaye ni mfanyabiashara katika Soko la Majengo, alisema kuwa ujenzi wa soko hilo utasaidia kukuza uchumi wao kwa kuwa watakuwa wanafanya biashara katika mazingira ya kisasa.
Naye Laurent Munish, ambaye pia ni mfanyabiashara katika soko hilo, aliipongeza Serikali kwa hatua ya kutatua changamoto zilizodumu kwa muda mrefu na kusababisha usumbufu kwa wafanyabiashara. Alisema changamoto hizo sasa zinaelekea kutatuliwa kupitia ujenzi wa soko jipya.
Akizungumzia ujenzi wa barabara ya Mkalama, Bw. Hamza Zuberi, mkazi wa eneo hilo, alieleza kuwa mradi huo utasaidia kuongeza thamani ya maeneo hayo na pia kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi.




