Tuesday, December 9, 2025
spot_img
HomeHabariMradi wa TACTIC kuchochea maendeleo kupitia barabara na stendi mpya Geita

Mradi wa TACTIC kuchochea maendeleo kupitia barabara na stendi mpya Geita

Mradi wa TACTIC unatekeleza ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 17 kwa kiwango cha lami katika Manispaa ya Geita, mkoani Geita, mradi unaotarajiwa kufungua mawasiliano na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.

Inadaiwa kuwa barabara hizo zitakuwa kichocheo cha biashara na shughuli mbalimbali za kijamii, hatua itakayoongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa manispaa na mkoa kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Bw. Yefred Myenzi, ameishukuru Serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi yenye kugusa moja kwa moja maisha ya wananchi.

“Ukiangalia kwa wigo mpana, miji inakua kwa kasi lakini kasi ya kujenga barabara na miundombinu yake ni ndogo. Tunapopata fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu, hasa ya barabara, ni fursa kubwa kwa wananchi kwa sababu inaboresha mandhari na muonekano wa mji wetu,” amesema.

Ameongeza kuwa ujenzi wa barabara hizo unahusisha pia uwekaji wa taa za barabarani, jambo litakalowezesha wananchi kufanya biashara hadi nyakati za usiku na pia kuimarisha usalama wa wananchi.

Kwa upande wake, Edward Misalaba, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwatulole, amesema ameridhishwa na ujenzi wa barabara ya Mkolani–Mwatulole na kueleza kuwa utekelezaji wake utachangamsha shughuli za mtaa huo na kuwa chachu ya biashara kwa wakazi wake.

Naye Faraja Magulu, Mama Lishe anayeendesha shughuli zake pembezoni mwa barabara hiyo, amesema ujio wa mradi huo ni neema kwao kwani utavutia watu wengi na kuongeza idadi ya wateja. Ameutumia fursa huo kuwataka kina mama wenzake kuchangamkia uwepo wa fursa mbalimbali za kibiashara.

Mbali na ujenzi wa barabara, mradi wa TACTIC pia unatekeleza ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi ya Mkoa wa Geita, ambao upo katika hatua za mwisho za utekelezaji wake.

Akizungumzia umuhimu wa mradi huo, Bw. Myenzi amesema stendi hiyo ni hitaji la muda mrefu kwa wananchi wa Geita na utekelezaji wake utaongeza mapato ya manispaa kwa kiasi kikubwa. Kwa mujibu wake, mapato ya kila siku yataongezeka kutoka shilingi 700,000 yanayopatikana sasa katika stendi ya sasa hadi kufikia shilingi 2,500,000, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 300.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments