Aliyekuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Joelson Mpina, ametenguliwa kugombea nafasi hiyo baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kubaini dosari katika mchakato wa uteuzi wa chama hicho.

Taarifa hiyo imekuja baada ya Monalisa, aliyewasilisha malalamiko kwa ofisi ya Msajili, kuonesha dosari za kikatiba na kikanuni katika uteuzi wa Mgombea Urais wa ACT Wazalendo. Baada ya kukutanishwa mbele ya Msajili pamoja na viongozi wa ACT Wazalendo wakiongozwa na Katibu Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa chama, leo Agosti 26, 2025, Msajili amekubaliana na hoja za Monalisa na kutoa maamuzi rasmi.
Hoja zilizothibitishwa ni pamoja na:
- Kanuni za Uchaguzi za ACT-Wazalendo za mwaka 2024 zinatumika pia katika kuteua wagombea wa nafasi za kiserikali, ikiwemo Urais. Hivyo, Mpina anakosa sifa ya kuwa mwanachama wa chama siku 7 kabla ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi.
- Mwisho wa kuchukua fomu za kuomba uteuzi ulikuwa tarehe 25 Mei 2025, wakati Mpina alijiunga na chama tarehe 5 Agosti 2025, siku moja kabla ya kutangazwa kwa Mkutano Mkuu wa chama tarehe 6 Agosti 2025. Hii inakiuka kanuni za chama ambazo zinataka ratiba ya fomu iendelee kwa utaratibu uliowekwa. Hakukuwa na ushahidi wa kikao chochote cha chama kilichorekebisha ratiba rasmi ya kuchukua na kurejesha fomu.
Kwa msingi huo, Msajili wa Vyama vya Siasa ametangaza wazi kuwa uteuzi wa Luhaga Mpina ni batili kisheria, na hivyo hastahili kuwa Mgombea Urais kupitia ACT Wazalendo.




