Mtu mmoja akamatwa kwa shambulio la Padri Kitima

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Rauli Mahabi kwa tuhuma za kujeruhiwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima.

Hatua ya kushikiliwa kwa Mahabi mkazi wa Kurasini, Dar es Salaam, imetolewa na Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam kupitia kwa SACP Jumanne Muliro.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo , Padri Kitima ameshambuliwa eneo la Kurasini, Temeke jijini Dar es Salaam zilipo ofisi za TEC makao makuu.

Taarifa ya Polisi iliyotolewa leo, Alhamisi Mei 1, 2025 na Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro imeeleza kuwa pamoja na kumshikilia lakini Mahabi anahojiwa kuhusu tukio hilo.

“Anashikiliwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo. Uchunguzi wa kina unaendelea ili hatua kali na za haraka zichulikuliwe kwa wahusika,” ameeleza.

Kuhusu taarifa ilivyopokewa, Muliro amesema tukio hilo limetokea saa nne usiku wa kuamkia leo maeneo ya Baraza la Maaskofu Tanzania Kurasini, Temeke jijini Dar es Salaam.

“Padri huyo inadaiwa tangu saa tatu asubuhi (jana Jumatano) walikuwa na kikao na viongozi wa dini mbalimbali na baada ya kikao kuisha saa 1 jioni alikwenda kwenye kantini yao ambapo aliendelea kupata kinywaji hadi saa nne na robo alipokwenda maliwatoni pembeni ya kantini hiyo ndipo alidai kushambuliwa kichwani na kitu butu na watu wawili,” imeeleza taarifa ya Muliro.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Padri Kitima amepelekwa Hospitali ya Aga Khan na anaendelea na matibabu.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *