Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kupitia kampasi yake ya Mloganzila, kinatarajia kuanza ujenzi wa kituo kikubwa cha huduma za kibingwa kwa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, mara baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi wa Kituo cha Umahiri cha Afrika Mashariki.

Kaimu Mkurugenzi wa Mradi huo, Dk. Rodrick Kisenge, alisema awamu ya kwanza ilihusisha mafunzo kwa wataalamu na tafiti za kisayansi. Alibainisha kuwa kituo hicho kitasaidia kutoa huduma bora za matibabu, kukuza utafiti na kuongeza idadi ya wataalamu wa moyo.
Kwa mujibu wa WHO, magonjwa ya moyo huua watu milioni 17.9 kila mwaka, sawa na asilimia 32 ya vifo vyote duniani. Dk. Kisenge alisema Afrika ina uhaba mkubwa wa wataalamu na vifaa tiba, hali inayosababisha watoto wengi kuchelewa kupata huduma.



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema ujenzi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa serikali na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya Sh bilioni 224, na utaifanya Tanzania kuwa kinara wa huduma za moyo Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Apolinary Kamuhabwa, na Mkuu wa MUHAS, Prof. David Mwakyusa, walisema mradi huo utapunguza mzigo wa magonjwa ya moyo na kukuza tafiti za ndani. Dk. Felix Bundala kutoka Wizara ya Afya aliongeza kuwa kituo hicho kitapunguza vifo vya watoto na vijana vinavyotokana na magonjwa ya moyo.







