Wednesday, December 10, 2025
spot_img
HomeAfyaMUHAS kutumia akili mnemba kuchunguza saratani ya shingo ya kizazi

MUHAS kutumia akili mnemba kuchunguza saratani ya shingo ya kizazi

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimepokea kompyuta kuu tatu za kisasa za ‘Lambda Vector’ zitakazotumika kuchakata taarifa na kurahisisha utambuzi wa magonjwa pamoja na matibabu kwa kutumia akili bandia.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 30, 2025, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh milioni 40 vimetolewa na Shirika la Global Health Labs (GHL) la Washington, Marekani, kwa ushirikiano na Bill & Melinda Gates Foundation na Gates Ventures.

Prof Kamuhabwa amesema kompyuta hizo zitasaidia kuboresha utambuzi wa magonjwa, kurahisisha kazi za madaktari, na kuboresha maisha ya Watanzania, hususan wale wanaoishi maeneo ya vijijini.

“Badala ya daktari kukaa na kusoma vipimo mwenyewe, mashine inaweza kuchakata taarifa na kutoa mpango wa matibabu kwa ugonjwa fulani kwa asilimia 95-98. Hii inarahisisha maisha ya daktari na mgonjwa,” amesema.

Aidha, Prof Kamuhabwa amesema teknolojia hiyo itarahisisha wagonjwa wa vijijini kutuma taarifa zao mapema badala ya kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali kubwa.

Mkuu wa Kitengo cha Vifaa Tiba MUHAS, Deogratias Mzurikwao, amesema kompyuta hizi mpya zina uwezo mkubwa zaidi ikilinganishwa na tisa zilizokuwa zikitumika awali.

“Tunazo tisa tayari, lakini hizi tatu mpya zina uwezo mkubwa zaidi na zitasaidia kuboresha utambuzi wa kansa ya titi na kuendeleza teknolojia ya utambuzi wa magonjwa ya moyo ambayo bado ipo kwenye majaribio,” amesema.

Kompyuta hizi mpya zinatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi ya kidijitali katika afya nchini, zikisaidia wataalamu kupata matokeo sahihi na ya haraka katika matibabu na utafiti.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments