Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya, Dk. Ntuli Kapologwe, amesema mbio za Reunion Fun Run, zilizoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa msimu wa tatu, zinalenga kuboresha miundombinu ya michezo chuoni humo huku zikihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa mazoezi kwa afya.

Akizungumza leo, Novemba 23, 2024, baada ya mbio hizo za kilomita 5, 10 na 15, Dk. Kapologwe alisema tukio hilo linaendana na kampeni ya kitaifa ya Mtu ni Afya chini ya mpango wa Fanya Kweli Usibaki Nyuma. “Mazoezi yanasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na mengineyo,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alieleza kuwa mbio hizo pia zinakusudia kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa michezo utakaohusisha viwanja vya basketi, netiboli, mpira wa miguu, gym ndogo, na kituo cha michezo kitakachosaidia wanafunzi na watumishi kuimarisha afya zao.




“Tunahitaji rasilimali za kutosha kufanikisha mradi huu, hivyo tunawaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia,” alisema Prof. Kamuhabwa.




Rais wa MUHAS, Marsha Macatta-Yambi, aliongeza kuwa uwanja mpya utasaidia kukabiliana na changamoto za magonjwa nyemelezi na kuimarisha afya ya jamii. “Pia, tunataka kuwapa heshima wanaochangia kufanikisha ujenzi huu kwa kuweka kumbukumbu maalum za majina yao,” alisema.
Pendo Paul, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Shahada ya Uuguzi, alihimiza jamii kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujilinda dhidi ya magonjwa na kuboresha maisha yao.
Mbio hizi zimedhihirisha mchango wa michezo si tu kwa afya binafsi bali pia katika kujenga miundombinu muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.














