Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimesema kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET), kimefanikiwa kuboresha mitaala 82 ya shahada ya uzamili na kuanzisha mitaala 23 ya programu mpya.

Hii ni sehemu ya juhudi za chuo katika kuboresha elimu na ufanisi wa masomo katika sekta ya afya na sayansi shirikishi. Vilevile, Muhas imefanikiwa kuboresha mtandao wa mawasiliano na matumizi ya mifumo ya kidigitali katika Kampasi ya Muhimbili.
Katika hafla ya mahafali ya 18 yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Dkt. Rehema Horera, amesema kwamba juhudi hizi zimedhihirika katika uboreshaji wa mafunzo ya wataalamu ambapo wanataaluma 33 wamepatiwa mafunzo ya uzamili na shahada za uzamiivu nchini na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo katika ufundishaji.
Pia, Dkt. Horera ameongezea kuwa, kitengo cha kuzalisha mapato na mpango wa biashara umeandaliwa na kupitishwa kwa ajili ya utekelezaji. Aidha, MUHAS imetengeneza na kuidhinisha sera za jinsia, ikiwa ni pamoja na Sera ya Kuzuia na Kupambana na Unyanyasaji wa Kijinsia na Sera ya Ujumuishaji wa Jinsia.




Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Apolinary Kamuhabwa, ametangaza kuwa jumla ya wahitimu ni 1,309, ambapo 461 ni wanawake, sawa na asilimia 35 ya wahitimu wote. Alisisitiza lengo la chuo kuwa ni kuwa na usawa wa kijinsia katika idadi ya wanafunzi na wahitimu.
Hafla hiyo ilishuhudia wahitimu 199 wakitunukiwa stashahada, 708 wakipata shahada ya kwanza, 441 wakipata shahada ya uzamili, na wengine 33 wakitunukiwa digrii za uzamili na bobezi, huku 8 wakipata digrii ya uzamivu ya udaktari wa falsafa.
Profesa Kamuhabwa pia ameelezea mafanikio ya programu mpya ya shahada ya uzamili na ubobezi kwenye uchunguzi wa magonjwa ya wanawake kwa kiradiolojia, ambapo wahitimu wawili wa kwanza walitunukiwa digrii mwaka huu wa 2024.
Mhitimu Satrumin Arbogast amewataka wahitimu wenzake kutumia changamoto kama njia ya kukua, akisisitiza umuhimu wa uvumilivu na ujasiri katika kufikia mafanikio. Mwanafunzi wa digrii ya uzamili, Katunzi Mutalemwa, aliwahimiza wahitimu kutumia ujuzi na umahiri waliosoma ili kutoa huduma bora na kuongeza umahiri katika sekta ya afya.
Chuo Kikuu cha Muhimbili kimeendelea kuwa kielelezo cha mafanikio katika sekta ya elimu ya juu, na juhudi hizi ni ishara ya mabadiliko makubwa katika ufundishaji na huduma za afya nchini Tanzania.




