
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), imerejesha tabasamu kwa mtoto Maliki Hashimu (6), mkazi wa Goba, Dar es Salaam, aliyekatwa koo na anayedaiwa kuwa ni dada wa kazi ‘hausigeli’.
Maliki, ametibiwa kwa miezi minne MNH, kwa matibabu yaligharimu Sh. milioni 15 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa msaada wa Rais Samia Suluhu Hassan.Â
Maliki, alipoteza sauti na kushindwa kuzungumza baada ya kupata majeraha shingoni na kuathiri koo lake, kutokana na kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni Julai mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi, amesema matibabu ya mtoto Maliki yamefanyika hatua kwa hatua na watalaam wamejiridhisha kwa kurejesha kila kilichokuwa kimepata hitilafu kwenye shingo yake na kwamba sasa yupo salama kuendelea na shule na maisha yake ya kawaida.
