Mwambusi aimarisha ulinzi Coastal Union, aitisha Yanga

KOCHA mpya wa Coastal Union, Juma Mwambusi, amesema ameanza na mazoezi maalumu ya kuisuka upya safu ya ulinzi ya timu hiyo ili isiruhusu mabao katika mechi dhidi ya Yanga itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Akizungumza na Nipashe jana, Mwambusi alisema amewataka wachezaji wake waingie katika mechi hiyo kwa tahadhari kwa sababu wanakutana na timu ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja. 

“Nataka kujenga heshima kwa kuifunga Yanga katika mchezo wetu huo ambao ninaamini utakuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa, timu hizi zinapokutana mchezo hauwezi kuwa mwepesi, mchezo huwa na ushindani wakati wote,” alisema Mwambusi. 

Kocha huyo alisema pia amefuatilia michezo iliyopita ya timu yake na kuongeza hajaridhishwa na kasi iliyokuwa inaonyeshwa na safu ya ushambuliaji, hivyo kuifanyia marekebisho ili ipate nafasi ya kuifunga Yanga. 

Aliongeza malengo yake ni kupata pointi tatu katika mchezo wake huo wa kwanza akiwa ndani ya kikosi hicho. 

“Tunaendelea vizuri na mazoezi, ninashukuru mpaka sasa hakuna mchezaji yoyote ambaye ni majeruhi jambo ambalo linampa matumaini makubwa. Kila mchezaji yuko tayari kwa mchezo huo wa Jumamosi, wanafahamu hautakuwa mwepesi kwa kila upande kutokana na historia ya timu hizi,” Mwambusi alisema.

Aidha Mwambusi amewaomba mashabiki wao kuendelea kujitokeza kuwashangilia kwa sababu hali hiyo inawaongezea hamasa ya kupambana kusaka matokeo mazuri.

“Tunaomba mashabiki waendelee kutupa ushirikiano, wajitokeze kwa wingi uwanjani ili tutimize mipango yetu, tumejipanga kuwapa furaha,” Mwambusi alisema.

Chanzo: Nipashe

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *