Monday, February 16, 2026
spot_img
HomeElimuNaibu Waziri aipongeza CBE kwa mageuzi ya kitaaluma

Naibu Waziri aipongeza CBE kwa mageuzi ya kitaaluma

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo amekipongeza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kwa mageuzi makubwa yaliyofanyika chuoni hapo na amekitaka pia kuweka mipango ya kusaidia wajasiriamali wadogo na wakati kurasimisha biashara zao.

Akizungumza chuoni hapo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea chuo hicho, Londo alisema wakati anaapishwa mkoani Dodoma Rais Samia Suluhu Hassan alimwambia kuwa moja ya majukumu anayopaswa kusimamia ni urasimishaji wa biashara za wajasiriamali.

“Tutafute namna ya kuwarasimisha bila kuwasumbua na lazima tuwaelimishe wasione kuwa kuwarasimisha ni njia ya kutaka kuwaingiza kwenye kulipa kodi, waondokane na mtazamo huo waone kwamba kurasimishwa ni njia ya kuleta tija kwenye biashara zao,”

“Wafanyabiashara hasa hawa wajasiriamali wanapaswa  kuona kuwa kurasimishwa kutawasaidia kuzalisha zaidi na kuyafikia masoko mengi ya ndani na nje ya nchi kwa urahisi na kujiongezea kipato,” alisema.

Pia Naibu Waziri alikipongeza chuo hicho kwa kuendelea kuongeza idadi ya machapisho ya kitaaluma akisema kuwa kufanya hivyo kunazidi kukiongezea hadhi chuo hicho kitaifa na kimataifa.

“Umahiri wa chuo ni wanataaluma wake kufanya tafiti nyingi zinazotoa majibu ya changamoto kwenye jamii na kutoa machapisho mengi ya kitaaluma, na eneo hili hapa CBE mnafanya vizuri sana hongereni sana kwa hilo,” alisema Naibu Waziri

Alikipongeza chuo hicho kwa kuimarisha uhusiano wake na vyuo mbalimbali duniani hali ambayo imewawezesha baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho kusoma masomo yao ndani ya nchi na kwenda kumalizia nchi za nje.

Naye Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa miongozo na maono yake ambayo chuo hicho imekuwa ikitekeleza na kuleta manufaa kwenye kuongeza udahili na ubora wa taaluma chuoni.

Alisema mpaka mwaka 2020 chuo hicho kilikuwa na wanafunzi 10,000 lakini mpaka kufikia mwaka 2025 udahili wa wanafunzi wa chuo hicho umeongezeka hadi kufikia 24,657 ambalo ni ongezeko la asilimia 135.

Alisema mwaka huu chuo hicho kimepata ithibati kwaajili ya kuanzisha program za uanagenzi ambapo mwanafunzi wa chuo hicho atasoma nusu ya masomo yake chuoni na nusu ya muda wake atautumia kwa mwajiri kufanya kwa vitendo.

Alisema wanatarajia kuanzisha shahada ya kwanza ya program ya kutafuta masoko kidijitali ambapo wanafunzi watakuwa wanajifunza kidijitali zaidi masuala ya masoko.

Alisema CBE pia imeshaanzisha Shahada za Uzamili mtandaoni  ambapo mwanafunzi anaweza kufanya masomo yake akiwa popote pale nchini bila kulazimika kuwa chuoni.

“Tunashukuru kuona Naibu Waziri ametutembelea na kuona mageuzi makubwa ambayo chuo kimefanya ikiwemo kukifanya chuo kiwe cha kimataifa, kuna wanafunzi wanaweza kusoma miaka miwili hapa na miaka miwili wakaenda kumalizia China na kwingineko,” alisema

“Naibu Waziri ametupa jukumu la kuangalia namna ya kusaidia kurasimisha biashara za wafanyabaishara wadogo na wakati ili waweze kuleta tija kwenye biashara zao tunakwenda kufanya tafiti tuone namba bora ya kulitekeleza hilo,” alisema

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments