NEMC yaanzisha operesheni kudhibiti kelele wakati wa sikukuu

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeunda timu maalumu ya operesheni kwa ajili ya kufuatilia na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wachafuzi wa mazingira na kelele kwenye kumbi za starehe msimu wa sikukuu.

Kaimu Mkurugenzi wa Utekelezaji wa Sheria wa NEMC, Jamal Baruti, alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema timu hiyo itafanya kazi katika kanda zote za NEMC nchini, hasa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, ambapo itashughulikia malalamiko ya kimazingira kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa, wananchi, na Jeshi la Polisi.

“Tutapokea taarifa muda wa saa 24 kupitia timu yetu maalumu ya kupokea taarifa (Call Centre Team) ili kufanyia kazi matukio ya uvunjifu wa sheria za mazingira,” alisema Baruti.

Baruti alihimiza taasisi, kampuni, na wananchi wote kufuata sheria na kanuni za mazingira, hasa kuhusu sauti na mitetemo inayozidi viwango pamoja na utiririshaji wa maji taka.

Alisema NEMC imeongeza juhudi za kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuheshimu sheria za mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Pia alisisitiza kuwa hatua za kiutawala na kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale watakaokaidi.

Hali ya uchafuzi wa mazingira, hususan kelele, mitetemo, na maji taka, imekuwa ikiongezeka katika miji yenye ukuaji wa haraka kiuchumi kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, na Pwani. Maeneo ya starehe na mikusanyiko ya watu yamekuwa kitovu cha changamoto hizi, hasa katika kipindi cha sikukuu.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *