NEMC yawataka wawekezaji kusajili miradi yao

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wawekezaji nchini kuzingatia sheria kwa kusajili miradi yao kwenye baraza hilo kabla ya kufanya uwekezaji wowote.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Afisa Mzingira wa (NEMC), Dalia Kilamlya, wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu mafanikio waliyoyapata kwenye maonyesho ya nanenane.

Maonyesho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Nzuguni Dodoma na katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya mazingita, wawekezaji wanapaswa kusajili miradi yao kwanza ili ifanyiwe tathmini ya athari kwa mazingira na kupewa cheti cha EIA ndipo waendelee na uwekezaji.

Alisema kwenye maonesho ya nane nane yaliyohitimishwa hivi karibuni walifanikiwa kuwafikia wadau 1,450 ambao wamewapa elimu ya uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira ikiwemo umuhimu wa kusajili miradi.

Alisema kwenye maonyesho ya nanenane walifanikiwa kutoa elimu kwa wadau kutoka sekta mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi za Baraza hilo kuhamasisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, alisema walifanikiwa kuelimisha kuhusu mbinu bora za kilimo hifadhi kinachozingatia mazingira, ufugaji endelevu, uvuvi salama pamoja na kulinda vyanzo vya maji.

Aidha, alisema wananchi na wadau waliotembelea banda la NEMC walielimishwa kuhusu umuhimu wa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ya kilimo ili kupunguza athari hasi kwa mazingira.

Alisema miongoni mwa masuala yaliyopatiwa kipaumbele ni pamoja na kuwahimiza wawekezaji kusajili miradi NEMC ili kupata vyeti vya mazingira kama kigezo muhimu cha kuendesha shughuli zao kisheria na kwa kuzingatia mazingira.

Alisema katika maonesho hayo ya mwaka huu, wataalamu wa NEMC pia walieleza athari za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za shughuli za binadamu kama uchomaji moto hovyo, ukataji miti na utupaji taka kwenye mifumo ya ikolojia.

Alisema vitendo kama hivyo vinachangia mabadiliko ya tabianchi kama vile mmomonyoko wa ardhi na upungufu wa rasilimali maji hivyo kusababisha ukame.

“Tunawahimiza wawekezaji kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira. Elimu tunayoitoa ni msingi wa kufanya maamuzi sahihi ya kisera, kiuchumi na kijamii yanayozingatia mustakabali wa mazingira yetu,” alisema

“Kwa ujumla, mwitikio wa wadau mbalimbali katika kupata elimu ya mazingira kutoka NEMC umekuwa mkubwa na wenye kuleta matumaini ya mabadiliko chanya katika namna jamii inavyoshiriki kwenye kulinda na kuhifadhi mazingira,” alisema.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *