Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeshiriki katika zoezi la utunzaji wa mazingira jijini Arusha kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo. Zoezi hilo liliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Irene C. Isaka, likiwahusisha watumishi wa NHIF kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, Dkt. Isaka alisema NHIF inatambua umuhimu wa kulinda mazingira na kuzingatia matakwa ya Umoja wa Mataifa kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan malengo namba 13 na 15 yanayosisitiza utunzaji wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Alieleza kuwa jitihada hizo pia zinaendana na maono ya Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amekuwa kinara katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini kama sehemu ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, sambamba na malengo yaliyoainishwa katika Dira ya Maendeleo 2050.
Zoezi hilo ni mwendelezo wa shughuli kama hiyo iliyofanyika mkoani Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2026, ambapo watumishi wanawake wa NHIF walishiriki kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Akizungumza na watumishi wakati wa shughuli hiyo, Dkt. Isaka alisema NHIF imedhamiria kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii kwenye eneo la utunzaji wa mazingira. Aliongeza kuwa mara nyingi mabadiliko makubwa huanza na hatua za watu wachache wanaothubutu kuanzisha.
“NHIF tunaonesha njia tukiwa na hamasa kwamba jamii nzima itaunga mkono juhudi hizi ili nchi yetu ifikie malengo ya maendeleo endelevu,” alisema Dkt. Isaka.
Kwa mujibu wa NHIF, zoezi la kupanda miti katika mikoa ya Dodoma na Arusha ni mwanzo tu, na litapanuliwa katika mikoa mingine yote nchini kutokana na mfuko huo kuwa na ofisi na watumishi katika kila mkoa.

Kwa upande wa Arusha, NHIF imepanda jumla ya miti 1,000 katika maeneo ya Hospitali ya Jiji iliyopo Njiro, Kituo cha Afya Moshono, Moivaro na Olmoti.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Jiji iliyopo Njiro, Said Salim, aliushukuru uongozi wa NHIF kwa kuchagua hospitali hiyo kupanda miti, akisema hatua hiyo itasaidia kuboresha mazingira ya hospitali na kuongeza ustawi wa wagonjwa pamoja na watumishi.
“Tunajiona wenye bahati kufikiwa na zoezi hili,” alisema Dkt. Salim.
NHIF imesisitiza kuwa itaendelea kuwa chachu ya mabadiliko katika utunzaji wa mazingira kote nchini kupitia shughuli kama hizi. 🌱🌍





