Friday, March 6, 2026
spot_img
HomeBiasharaNMB, PPRA waja na mfumo uhakiki dhamana za zabuni kidigitali

NMB, PPRA waja na mfumo uhakiki dhamana za zabuni kidigitali

Benki ya NMB kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) wamezindua huduma mpya ya kidijitali ya Uhakiki wa Dhamana za Zabuni za Kibenki (Digital Bank Guarantee Verification).


Huduma hiyo itafanya kazi kupitia Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Kielektroniki Tanzania (NeST), hatua inayotarajiwa kurahisisha michakato ya zabuni na kuimarisha uwazi katika matumizi ya fedha za umma.

Uzinduzi wa huduma hiyo ulifanyika jijini Dar es Salaam jana, ambapo Benki ya NMB iliweka rekodi ya kuwa taasisi ya kwanza ya fedha nchini kutoa huduma ya dhamana za zabuni kwa mfumo wa kidijitali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema hatua hiyo inalenga kuboresha mfumo wa utoaji na uthibitishaji dhamana za benki katika michakato ya ununuzi wa umma, ambayo ni moja ya nguzo muhimu za shughuli za kiuchumi nchini.

Alisema kila siku kampuni kubwa, biashara ndogo na za kati (SME), makandarasi, wasambazaji na watoa huduma hushiriki katika zabuni za serikali zinazohitaji kasi, uaminifu na uzingatiaji taratibu za kisheria.

Kwa mujibu wa Zaipuna, kwa muda mrefu mchakato wa dhamana za benki katika ununuzi wa umma ulikuwa ukikabiliwa na changamoto kadhaa ukiwamo utegemezi mkubwa wa nyaraka za karatasi, ucheleweshaji uthibitishaji pamoja na hatari ya udanganyifu au kupotea kwa nyaraka muhimu.

“Kwa kushirikiana na PPRA, tumekuja na huduma hii inayowezesha wateja kuwasilisha na kuthibitisha dhamana za benki papo hapo kupitia mfumo wa kidijitali. Hii itarahisisha michakato ya zabuni na kuongeza ufanisi katika sekta ya ununuzi wa umma,” alisema.

Aliongeza kuwa huduma hiyo itasaidia kupunguza muda uliokuwa ukitumika kukamilisha michakato ya uthibitishaji dhamana za zabuni, ambao wakati mwingine ulikuwa ukichukua siku kadhaa.

Kwa mujibu wake, kwa kutumia mfumo huo mpya, mchakato huo sasa unaweza kukamilika kwa muda mfupi, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi kwa kampuni na taasisi zinazoshiriki katika zabuni za serikali.

Zaipuna alisema huduma hiyo pia itawarahisishia wazabuni kuwasilisha aina mbalimbali za dhamana za benki bila kulazimika kupitia taratibu ndefu za kiutawala.

Alitaja baadhi ya manufaa ya huduma hiyo kuwa ni pamoja na kushiriki zabuni kwa haraka zaidi, uthibitishaji dhamana kwa wakati, kupunguza mzigo wa ufuatiliaji nyaraka pamoja na kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika michakato ya zabuni.

“Huduma hii pia itaongeza kiwango cha uaminifu kwa wazabuni na taasisi nunuzi wakati wa kushindania zabuni, kwani kila hatua itakuwa ikithibitishwa moja kwa moja kupitia mifumo ya kidijitali,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, aliipongeza NMB kwa kuchukua hatua hiyo ambayo alisema inaendana na maono ya serikali ya kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji huduma za umma.

Alisema hatua hiyo pia inaunga mkono juhudi za serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha mifumo ya taasisi mbalimbali inasomana ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali.

Simba alisema kwa kuunganishwa kwa mfumo wa NeST na mifumo ya benki, taasisi nunuzi hazitalazimika tena kuwasiliana moja kwa moja na benki ili kuthibitisha uhalali wa dhamana za zabuni zinazowasilishwa na wazabuni.

Badala yake, mzabuni atahitajika kuweka namba ya dhamana aliyopewa na benki, na mfumo wa NeST utaweza kuipata na kuithibitisha moja kwa moja kutoka kwenye mfumo wa benki husika.

“Mapinduzi haya yataondoa kabisa ucheleweshaji uliokuwa ukitokea wakati wa taasisi nunuzi kutafuta uthibitisho wa dhamana za benki. Mfumo utakuwa ukisomana moja kwa moja na benki,” alisema.

Kwa sasa mfumo wa NeST unasomana na taasisi zaidi ya 20, na ujio wa huduma hiyo unatarajiwa kuimarisha zaidi ufanisi katika utekelezaji michakato ya zabuni za serikali.

Simba alisema ununuzi wa umma ni nyenzo muhimu katika utekelezaji miradi ya maendeleo ya taifa, hivyo ni muhimu kuhakikisha mifumo inayosimamia michakato hiyo ina uwazi, ufanisi na usalama wa kutosha.

Alieleza kuwa dhamana za kifedha kama dhamana za zabuni, dhamana za utekelezaji mikataba na dhamana za malipo ya awali zina jukumu muhimu katika kuhakikisha wazabuni na wakandarasi wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa makubaliano.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments