Benki ya NMB Plc imeorodheshwa miongoni mwa Benki 40 Bora barani Afrika, ikiendelea kuwa Benki Namba Moja Tanzania na benki pekee ya Tanzania katika orodha ya Benki Tano Bora Afrika Mashariki.
Orodha hii ya mwaka 2025 imetolewa na jarida la African Business lenye makao makuu London, Uingereza.
Utambuzi huu unaonesha kupanda kwa NMB kwa uthabiti kama mojawapo ya taasisi za kifedha zenye ustahimilivu na nguvu zaidi Afrika, iliyojengwa juu ya misingi imara, utawala thabiti na utekelezaji wa nidhamu wa mkakati wa ukuaji wa muda mrefu.
Uwekaji orodha ulizingatia mtaji wa jumla, mali ya jumla na uwezo wa kuzalisha faida, ukithibitisha nguvu na uendelevu wa benki katika mazingira magumu ya kikanda na kimataifa.
Juni 2025, jumla ya mali ya Benki ya NMB ilizidi Sh. trilioni 14, inayotokana na msingi imara wa mtaji, ukwasi na kiwango cha ukuaji wa kila mwaka cha zaidi ya asilimia 30 katika faida halisi kwa kipindi cha miaka mitano. Faida kwa hisa ya benki inabaki kuwa ya juu zaidi Afrika Mashariki, ikiashiria ugawaji wa mtaji kwa ufanisi na mbinu bora za usimamizi.
Mafanikio haya yanatokana na utekelezaji kwa mafanikio Mpango Mkakati wa Muda wa Kati wa 2021-2025, uliokuwa na lengo la kuendeleza ushirikishwaji kifedha, mabadiliko ya kidijitali, ufanisi wa utendaji na uendelevu.
Leo, zaidi ya asilimia 96 ya shughuli zote za wateja zinafanyika nje ya matawi, ambayo ni athari chanya ya uwekezaji wa kimkakati katika teknolojia na uzoefu wa wateja.
Zaidi ya utendaji na uimara wa kifedha, NMB imeendelea kuongoza kama benki yenye uwajibikaji na uendelevu. Mwaka 2021, Benki ya NMB iliandika historia kama benki ya kwanza Afrika kutoa Hati Fungani ya Jasiri, ikidhihirisha dhamira yake ya fedha jumuishi na uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake.
Mafanikio hayo yalifanya Benki ya NMB kupata Tuzo ya Hati Fungani Endelevu ya Mwaka iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) na Jukwaa la Kufadhili Ujasiriamali (SME Finance Forum), ushahidi wa uongozi wa benki katika kuendeleza ukuaji endelevu na wa haki kote barani.
NMB pia imepata tuzo mbalimbali za kimataifa pamoja na Benki Bora ya Uendelevu Barani Afrika kutoka Jarida la Euromoney la nchini Uingereza, cheti cha Mwajiri Bora kwa ubora mazingira ya kazi na Cheti cha EDGE kwa usawa wa kijinsia, ikawa benki ya kwanza Afrika kufikia hatua hii muhimu.
Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, alisema: “Utambuzi huu unadhihirisha nguvu ya mkakati wetu, ustahimilivu wa watu wetu, na imani ambayo wateja wetu wanaweka kwetu. Ni wakati wa fahari kwa Tanzania na ukumbusho wa wajibu wetu wa kuendelea kujenga taasisi ya kifedha yenye viwango vya kimataifa inayotoa thamani endelevu kwa wadau wote.”
Ujumuishaji wa Benki ya NMB kati ya benki 40 Bora Barani Afrika unadhihirisha kuwa ni taasisi Imara, endelevu, inayotazama mbele na inayoendesha ukuaji jumuishi na tekinolojia.
“Mafanikio haya tunayapeleka kwa wadau wetu ambao wamekuwa nasi katika safari hii,” ilisoma sehemu ya taarifa ya benki kwa umma. “Kwa pamoja, si tu tunaijenga benki bali tunabadilisha maisha na kuweka misingi imara ya kifedha kwa vizazi vijavyo vya Tanzania na Afrika kwa Ujumla,” alisema Zaipuna.
Benki ya NMB Plc ni taasisi ya kifedha iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam na inayohudumia zaidi ya wateja milioni tisa kote nchini kupitia mtandao wa matawi, wakala wa benki, na majukwaa ya kidijitali.




