Sunday, December 21, 2025
spot_img
HomeHabariOSHA ina nafasi muhimu ya kuwezesha shughuli cha uzalishaji-Katibu Mkuu Kazi

OSHA ina nafasi muhimu ya kuwezesha shughuli cha uzalishaji-Katibu Mkuu Kazi

Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mary Maganga, amesema Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ni Taasisi yenye umuhimu na nafasi kubwa katika kuwezesha shughuli za uzalishaji kufanyika kwa tija.

Ametoa kauli hiyo wakati akifungua Kikao cha Tano cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika jana (Desemba 20, 2025) Jijini Dodoma ambapo Katibu Mkuu huyo alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kikao hicho.

Aidha, Katibu Mkuu huyo ameipongeza OSHA kwa kutekeleza ipasavyo jukumu lake la msingi la usimamizi wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ambapo amewasisitiza watumishi kuendelea kufanya kazi kwa weledi kwa kadri ya kanuni za utumishi wa umma pamoja na kuimarisha ushirikiano baina yao.

“Kabla ya kufungua rasmi kikao hiki, ninaomba nisisitize mambo machache; kwanza niwatake kufanya kazi kwa weledi kwani mara nyingi tumekuwa tukiamini kwamba wito unahusiana na shughuli za viongozi wa dini pekee lakini tunasahau kwamba hata hizi kazi zetu ni wito kwakuwa kuna majukumu ambayo ni lazima tuyafanye kwa ajili ya watu ambao wanategemea sana huduma zetu,” ameeleza Maganga.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu kufungua kikao, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema kikao hicho kinalenga kutathmini utendaji wa Taasisi ya OSHA kwa kutazama kipindi kilichopita, kilichopo ili kupata mustakabali wa maendeleo ya OSHA katika kipindi kijacho.

“Kikao hiki pamoja na kutathmini utendaji wa Taasisi kwa mwaka wa fedha uliopita (2024/2025) kinalenga kuangalia mwenendo wa utendaji wetu katika miezi mitano iliyopita ya mwaka huu wa fedha (2025/2026) hususan katika kipindi hiki tunapoelekea kuandaa bajeti ya mwaka wa fedha ujao (2026/2027),” amesema Mtendaji Mkuu.

Alieleza kuwa kikao hicho kilitanguliwa na mafunzo kwa watumishi wote wa OSHA katika masuala ya maadili ya utumishi wa umma, mpango mkakati wa Taasisi wa miaka mitano ijayo (2026/2027-2030/2031), masuala ya afya ya akili pamoja na masuala ya itifaki.

Akiwasilisha salamu za wafanyakazi katika ufunguzi wa kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) ambacho wafanyakazi wa OSHA ni miongoni mwa wanachama wake, Rugemalila Rutatina, ameipongeza OSHA kwakuwa na utaratibu mzuri wa ushirikishwaji watumishi wote pasipo ubaguzi katika kufanya maamuzi ya masuala muhimu yanayohusu utendaji wa Taasisi hiyo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments