Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umezindua mpango wake wa kushirikiana na Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya katika kuwezesha biashara na uwekezaji nchini.
Mpango huo unahusisha utaratibu wa kuunganisha mifumo na kubadilishana taarifa za biashara na miradi mbalimbali ya uwekezaji ili kurahisisha ufikishaji wa huduma za urasimishaji biashara na ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi.
Mpango huo wa OSHA umewekwa wazi na Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Khadija Mwenda, alipohitimisha semina ya kujenga uelewa wa pamoja baina ya OSHA na Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya zote za Kanda ya Kaskazini ambao umefanyika kwa siku moja katika Ofisi za OSHA zilizopo Jengo la PAPU Jijini Arusha.
Mwenda amesema mpango huo umeibuliwa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akielekeza Taasisi za serikali kushirikiana katika utendaji ikiwemo kuhakikisha kwamba mifumo mbalimbali ya serikali inasomana.


Aidha, ameeleza kuwa mpango huo unalenga kutekeleza agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, alilolitoa Desemba 22, 2025 ambapo aliwataka waajiri/wamiliki wa maeneo ya kazi kote nchini kuhakikisha maeneo yao ya kazi yanasajiliwa OSHA ndani ya siku 90 kuanzia mwezi Januari 2026 ili kurahisisha usimamizi wa masuala ya usalama na afya katika maeneo husika.
“Lengo kuu la mpango huu ni kuhakikisha kuwa Taasisi ya OSHA inafanya kazi kwa kushirikiana na wenzetu ambao ni Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya wote tukiwa kama Taasisi wezeshi katika biashara na uwekezaji,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA na kuongeza:

“Tumekuwa na kikao kizuri sana ambacho kimetufungulia zoezi letu ambalo tumepanga kulifanya nchi nzima. Mpango huu utakapokamilika sote tutakuwa na uelewa wa pamoja ambao utapelekea taasisi zetu kuwa wawezeshaji zaidi badala ya kuwa wadhibiti wa shughuli za biashara na uwekezaji nchini.”
Kwa upande wao washiriki wa semina hiyo ambao ni Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya zote za Kanda ya Kaskazini ikihusisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga, wamepongeza mpango huo na kuahidi kushirikiana na OSHA kufanikisha mpango huo.
“Tumefurahia sana mafunzo ya leo,hakika tumetoka na ufahamu mpana kuhusiana na kazi za OSHA na tumeona kuna umuhimu mkubwa sana kwa wafanyabiashara na wawekezaji kujisajili katika mfumo rasmi ili waweze kuweka salama sehemu zao za kazi,” ameeleza Elisha Erasto, Mkuu wa Idara ya Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo.
“Tunaishukuru sana OSHA kwa semina ya leo na kwaniaba ya washiriki wenzangu ninapenda kusema kwamba tutashirikiana na OSHA ili kufanikisha mpango huu unaolenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na hivyo kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa 2050,” amesema Lulu Kaaya, Afisa Biashara Mkoa wa Arusha.
OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) yenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 inayoweka utaratibu wa kitaifa wa usimamizi wa masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi.






