Wadau wa pikipiki nchini wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kuzinduliwa rasmi kwa pikipiki mpya zenye unafuu mkubwa aina ya Daima na Everlast, zilizozinduliwa Jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huo uliofanyika katika viwanja vya TCC Club Chang’ombe, uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh. Albert Chalamila, aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mapunda aliipongeza Kampuni ya Alternative Solution Limited, wasambazaji wa pikipiki hizo, kwa uthubutu wao wa kuwaletea Watanzania bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya sekta ya usafirishaji.
“Inapendeza kuona sisi Watanzania tukitafuta suluhisho ili kuleta unafuu katika sekta hii ya usafirishaji. Pikipiki ni usafiri unaotegemewa sana nchini, hasa katika kusafirisha abiria na mizigo,” alisema Mapunda.
Aliwataka waendesha bodaboda kuzingatia sheria za barabarani na kufuata ushauri wa wataalamu ili kuhakikisha matumizi salama na kudumu kwa pikipiki hizo. Vilevile, aliomba mashirika ya kifedha kushirikiana na Alternative Solution Limited kuweka utaratibu wa mikopo nafuu kwa waendesha bodaboda ili kuwasaidia kumiliki pikipiki zao kwa njia rahisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Alternative Solution Limited, Bw. Ruge Chacha, alisema kampuni hiyo ilifanya utafiti wa kina kabla ya kuagiza pikipiki hizo ili kujua mahitaji ya watumiaji wa pikipiki nchini.
Alibainisha kuwa pikipiki za Daima na Everlast zimeboreshwa kwa viwango vya juu, zikiwa na:
- Nafasi kubwa ya kukalia kwa dereva na abiria
- Sehemu ya kubebea mizigo
- Sehemu ya kuchajia simu
- Sehemu ya kuwekea chupa ya maji
- Taa imara zinazoona vizuri hata wakati wa mvua na giza
- Matairi imara yanayoweza kubeba mzigo mzito bila wasiwasi
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau zaidi ya 300 wa sekta ya usafirishaji, ambapo baadhi walipata fursa ya kujaribu pikipiki hizo na kuuliza maswali kuhusu matumizi yake.
Mbunge wa Jimbo la Temeke, Mh. Dorothy Kilave, aliwataka waendesha bodaboda kuzingatia sheria za barabarani na kuhamasisha ununuzi wa pikipiki za Daima na Everlast kwa kuwa ni bidhaa bora zitakazosaidia kuboresha huduma za usafirishaji.
Baada ya uzinduzi huo, pikipiki hizo zitasambazwa nchi nzima kupitia mawakala mbalimbali wa kampuni hiyo.
