Tuesday, December 9, 2025
spot_img
HomeBiasharaPIKU Afrika yaendelea kunogesha minada ya kidijitali, yatoa zawadi kwa washindi

PIKU Afrika yaendelea kunogesha minada ya kidijitali, yatoa zawadi kwa washindi

Mambo yanazidi kushika kasi katika jukwaa la kidijitali la PIKU Afrika, linalojihusisha na uendeshaji wa minada ya kipekee kupitia mtandao, baada ya kuendelea kukabidhi zawadi kwa washindi wa awamu ya tatu ya promosheni yake.

Katika hafla hiyo, washindi watatu bora waliibuka na zawadi mbalimbali na kufanya jumla ya washindi waliopata zawadi kufikia tisa tangu promosheni hiyo ianze.

Walioshinda katika awamu hii ni Jakson Ngonji, aliyejinyakulia televisheni janja ya inchi 55 kutoka kampuni ya LG pamoja na ruta yenye kifurushi cha intaneti cha mwaka mzima. Mshindi wa pili, Jonathan Paul, alipokea kifurushi cha bidhaa za kiume ikiwemo pafyumu, vidani vya mkononi na saa ya kisasa, huku nafasi ya tatu ikinyakuliwa na Niovita Shayo, aliyeondoka na simu janja aina ya Samsung pamoja na spika ya Bluetooth.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa PIKU Afrika, Barnabas Mbunda, alisema kuwa hatua ya kuona zaidi ya washindi tisa wamenufaika tayari ni mafanikio makubwa kwa kampuni hiyo.

“Kwa PIKU Afrika, hili ni jambo la fahari kwani washindi wetu hupokea bidhaa zao bila kikwazo chochote. Hali hii inaonyesha uwazi na ubunifu wa mfumo wetu wa minada ya kidijitali,” alisema Mbunda.

Mbunda alifafanua kuwa zawadi mbalimbali hutolewa kwa washindi, ikiwemo bidhaa bora kwa bei nafuu na ya kipekee. Pia aliongeza kuwa bidhaa zote za kielektroniki ambazo zimeshinda tayari zimekatiwa bima ya mwaka mzima, jambo linalowapa washindi uhakika wa usalama na uimara wa bidhaa walizopokea.

Aidha, alibainisha kuwa promosheni hiyo bado inaendelea na minada mikubwa zaidi ipo njiani, huku akitaja zawadi kuu ya funga mwaka kuwa ni gari aina ya Toyota Raum litakalokabidhiwa pamoja na mafuta lita 100 kila mwezi kwa mwaka mzima, matengenezo ya bure kwa mwaka mmoja, na bima kamili ya mwaka mzima. Vilevile, mshindi mwingine atakabidhiwa pikipiki mpya aina ya TVS, ikiwa na helmeti na reflector, kadi ya mafuta lita 30 kila mwezi kwa mwaka mzima, pamoja na bima ya mwaka mzima.

Kuhusu ushiriki, Mbunda alisema tiketi za mnada hupatikana kwa gharama nafuu; Sh. 1,000 kwa tiketi 10, Sh. 5,000 kwa tiketi 50, Sh. 10,000 kwa tiketi 100, na Sh. 100,000 kwa tiketi 1,000. Alisisitiza kuwa kadri idadi ya tiketi inavyoongezeka, ndivyo nafasi ya kushinda inavyoongezeka.

Kwa upande wake, mshindi wa kwanza wa televisheni janja ya inchi 55, Jakson Ngonji, alieleza kwa furaha namna alivyonufaika kwa dau dogo kupitia mfumo wa kidijitali wa PIKU Afrika.

“Nilishiriki kwa matumaini na hadi sasa bado siamini kama kweli nimeshinda. Nawahamasisha Watanzania, hususan vijana, wajitokeze kushiriki minada hii kwa kuwa ni fursa ya kipekee ya kupata bidhaa za thamani kubwa kwa gharama ndogo,” alisema Ngonji.

Kwa ujumla, PIKU Afrika imeendelea kujidhihirisha kama kinara katika mapinduzi ya minada ya mtandaoni, ikiwapa Watanzania nafasi ya kupata bidhaa bora kwa bei nafuu kupitia mfumo wa kidijitali, wa uwazi, na wa kipekee.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments