Morogoro, Julai 18, 2025
Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Morogoro, ACP Samuel Kijanga, ametoa wito kwa wamiliki wa kampuni za ulinzi kuhakikisha wanaajiri vijana wenye nguvu na uwezo wa kiutendaji ili kuongeza ufanisi katika kazi ya ulinzi na usalama wa maeneo mbalimbali.

ACP Kijanga ametoa kauli hiyo leo alipokutana na wamiliki wa kampuni 23 za ulinzi kutoka Manispaa ya Morogoro katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa JKT Umwema.
Amesisitiza kuwa kampuni za ulinzi zinapaswa kufanya mazoezi na mafunzo ya mara kwa mara kwa walinzi wao ili waweze kukabiliana ipasavyo na wahalifu, kulinda mali, na kuimarisha usalama wa jamii inayowazunguka.
“Ni muhimu kuwaajiri vijana wenye nguvu na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiusalama. Wazee hawana wepesi wa kutosha kuhimili mikikimikiki ya uhalifu wa sasa,” alisema ACP Kijanga.


Aidha, amewashauri wamiliki wa kampuni hizo kuwahamasisha wateja wao kufunga kamera za ulinzi (CCTV) ili kusaidia kutunza kumbukumbu na kusaidia uchunguzi endapo tukio la kihalifu litajitokeza.
Kwa upande wake, Lukas Kaberenge, mmiliki wa kampuni ya Quick Security, amesema maelekezo na elimu waliyopewa na Jeshi la Polisi yamewafungua macho na kuwasaidia kubadilika ili kuendesha kampuni zao kwa njia za kisasa.
“Tumejifunza mambo mengi muhimu ambayo yatasaidia kampuni yetu kuwa ya kisasa zaidi, yenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya usalama katika mazingira ya sasa,” alisema Kaberenge.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa litaendelea kushirikiana na kampuni binafsi za ulinzi kwa karibu zaidi, kwa kuwa ni wadau muhimu katika mfumo wa ulinzi shirikishi unaolenga kulinda maisha na mali za wananchi.

