Friday, November 14, 2025
spot_img
HomeGeneral NewsWatangazaji wanne wa Mjini FM wapigwa marufuku na Bodi ya Ithibati

Watangazaji wanne wa Mjini FM wapigwa marufuku na Bodi ya Ithibati

Dar es Salaam, Julai 18, 2025
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imewachukulia hatua kali watangazaji wanne wa kituo cha redio cha Mjini FM kwa kosa la kufanya kazi za kihabari bila kusajiliwa na kukiuka maadili ya taaluma ya habari.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Bodi hiyo imesema kuwa watangazaji hao wamepigwa marufuku kujihusisha na kazi yoyote ya kihabari baada ya kubainika kuvunja misingi ya maadili ya uandishi wa habari, hasa katika kipindi cha mahojiano waliyofanya na msanii wa muziki wa Singeli, Dogo Paten.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mahojiano hayo yaliyopeperushwa hewani yalikiuka haki ya faragha ya mhojiwa, kumvunjia heshima, na kumshushia hadhi hadharani, jambo linalokwenda kinyume na misingi ya weledi, utu na uwajibikaji unaotakiwa kufuatwa na wanahabari wote waliosajiliwa kihalali.

“Watangazaji hao walikiuka kanuni za maadili ya taaluma ya habari kwa kufanya mahojiano yasiyo ya staha, yaliyojaa dhihaka na udhalilishaji dhidi ya mhojiwa. Aidha, walikuwa wakifanya kazi bila kusajiliwa, jambo ambalo ni kinyume na sheria ya Ithibati ya Waandishi wa Habari,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Bodi imeeleza kuwa marufuku hiyo ni ya muda usiojulikana hadi hapo watakapokidhi vigezo vya usajili na kuonyesha mabadiliko ya mwenendo wa kimaadili.

Aidha, Bodi imetoa wito kwa vyombo vyote vya habari nchini kuhakikisha kuwa wanatekeleza wajibu wao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya taaluma ya habari, huku wakiheshimu utu na haki za watu wanaoshiriki katika vipindi vyao.

“Kazi ya uandishi wa habari si ya kufanya kwa mazoea wala kwa ajili ya kiki. Ni taaluma inayohitaji weledi, uadilifu, na heshima kwa binadamu wote,” imesisitiza Bodi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments