Maafisa Rasilimaliwatu na Utumishi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Katavi wakiwemo wale wa Serikali Kuu pamoja na Wahasibu, wamesema Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ni chombo kinachowafanya kuwa na maisha ya uhakika hata baada ya kustaafu utumishi.
Kauli hiyo imetolewa na Shukuru Mwakaruka wakati akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi baina ya maafisa hao na Mfuko wa PSSSF mjini Mpanda.
Kikao hicho ambacho kimefanyika mjini Mpanda Septemba 16, 2025, ni sehemu ya mkakati wa Mfuko, kuwafikia wadau mbalimbali ili kuwajengea uelewa wa utekeelezaji wa majukumu ya Mfuko ambapo kundi la maafisa hao ndio kiungo muhimu baina ya Mfuko na watumishi ambao ni wanachama wa PSSSF.


“Tunatoka hapa tukiwa na uelewa mpana na tunakwenda kubadilisha elimu tuliyoipata kwenda kwenye vitendo ili kuwasaidia watumishi wenzetu.” Alisema Bw. Mwakaruka ambaye ni Afisa Rasilimaliwatu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Mkoani Katavi.
Naye Mrakibu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Katavi, John Mpangala, yeye alisema, licha ya kufurahishwa na maboresho yaliyofanywa na Mfuko hususan matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma, amepongeza hatua ya Mfuko kuwafikishia elimu maafisa Rasilimaliwatu kwenye Halmashauri na mikoani.
” Sisi maafisa wa chini ndio tunaoshughulika na Watumishi, hivyo nishauri elimu hii isambae hadi ngazi za chini.” alisisitiza.


Awali Afisa Mfawidhi wa PSSSF, Mkoa wa Katavi, Paul Mbijima, alisema Mfuko unawategemea sana maafisa Rasilimaliwatu kwani wao ni kiungo baina ya Watumishi (wanachama) na Mfuko.
” Tumekutana hapa leo ili kuwaeleza utekelezaji wa majukumu ya Mfuko na maboresho makubwa yaliyofanywa ikiwemo matumizi ya mtandao katika utoaji wa huduma zetu.” alisema.
Alisema, kwa zaidi ya asilimia 95 ya huduma za PSSSF zinatolewa kupitia mtandao wa PSSSF Kidijitali.
“Kupitia Mfumo, Mwanachama anaweza kujisajili, kuwasilisha Michango, Kuwasilisha Madai na kwa Wastaafu wanaweza kujihakiki kupitia simu janja.” alifafanua.
Pia aliwaeleza kuhusu uboreshaji wa Pensheni za Kila mwezi, ambapo kuanzia Januari 2025, Wastaafu waliokuwa wanalipwa kima cha chini cha pensheni ya sh. 100,000/= sasa wanalipwa sh. 150,000/= .





