Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umepongezwa kwa kuwa mdau muhimu katika kuimarisha ajenda za Kitaifa na ustawi wa jamii, kufuatia hatua yake ya kudhamini Mkutano wa 110 wa Waandaaji wa Maudhui- WASHITIRI.
Akifungua mkutano huo leo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Nchemba, aliipongeza PSSSF kwa kuonesha uzalendo wa hali ya juu kwa kuwa mdhamini mkuu wa mkutano huo jambo ambalo litasaidia kuimarisha amani kama ambavyo kauli mbiu inasisitiza, Sisi ni Tanzania, Taifa moja, Lengo moja.
“Nitoe pongezi za kipekee kwa PSSSF kwa kuwa mdhamini mkuu wa mkutano huu. Huu ni ushahidi tosha wa namna mifuko yetu inavyosaidia katika kufanikisha ajenda za Kitaifa, mchango mlioutoa tunaendelea kuuthamini sana, Mwenyekiti (PSSSF) tunakushukuru sana na wadhamini wote,” alisema Mhe. Nchemba.


Mwakilishi wa PSSSF, Meneja wa Kanda ya Ilala, Bi. Amina Kassim, alibainisha kuwa uamuzi wa kudhamini mkutano huo ni sehemu ya mkakati wa Mfuko katika kuwahudumia Watanzania kwani amani ya kweli inachochewa na mwananchi kupata huduma stahiki kwa wakati, jambo ambalo Mfuko unalitekeleza kwa weledi mkubwa.
“Tumedhamini mkutano huu ili kusogeza huduma karibu zaidi na wanachama wetu, asilimia kubwa ya washiriki wa mkutano huu ni wanachama wetu. Tunaamini kuwa amani inaimarika pale mwananchi anapopata huduma nzuri, kwa wakati, na popote alipo,” alieleza Bi. Amina.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Bw. Gwakisa Mlawa, aliipongeza PSSSF kwa kuwezesha mkutano huo uliowakutanisha washiriki takriban 250 kutoka taasisi mbalimbali za umma. Naye Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Paul Makonda, aliongeza kuwa msaada wa PSSSF utasaidia kuimarisha amani.





