PSSSF yashiriki Maonesho ya Wiki ya Afya na Usalama Kazini Kitaifa Singida

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unashiriki katika Maonesho ya Wiki ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSH – Occupational Safety and Health) yanayofanyika kitaifa kwenye Viwanja vya Maonesho Mandewa, mkoani Singida kuanzia Aprili 24 hadi 30, 2025.

Akizungumza kuhusu ushiriki huo, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa PSSSF, Rehema Mkamba, amesema maonesho haya ni jukwaa muhimu kwa mfuko huo kukutana moja kwa moja na wanachama pamoja na wananchi kwa lengo la kuwahudumia na kuwapatia elimu kuhusu matumizi ya teknolojia katika kupata huduma – maarufu kama PSSSF Kidijitali.

“Maonesho haya ni fursa adhimu ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zetu, lakini pia kuwaelekeza namna ya kutumia teknolojia ya kidijitali katika kujihudumia wao wenyewe mahali popote na wakati wowote,” alisema Mkamba.

Aidha, ameeleza kuwa kwa sasa PSSSF inaendesha zoezi la kuchukua alama za vidole kwa wanachama wake wote ili kuboresha zaidi huduma za kidijitali, hasa kwa madhumuni ya usalama na uthibitisho wa taarifa za wanachama.

Katika kuendana na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia za Kidijitali katika Kuimarisha Usalama na Afya Mahali pa Kazi”, PSSSF imejipanga kuhakikisha kuwa huduma zote muhimu zinapatikana kwa njia ya kidijitali.

Kupitia mfumo wa PSSSF Kidijitali, mwanachama anaweza kutumia simu janja, kishikwambi au kompyuta kuangalia taarifa za michango, mafao, uwekezaji, kuwasilisha madai mbalimbali mtandaoni, pamoja na huduma ya kujihakiki kwa wastaafu kupitia simu zao.

“Tunawakaribisha sana wanachama wetu pamoja na wananchi kutembelea banda letu, ili waweze kuelimishwa kuhusu huduma zetu za kidijitali na kupata huduma mbalimbali kwa urahisi zaidi,” alisisitiza.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *