Katika kusherehekea siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika kuanzia Machi 1 na kufikia kilele Machi 8, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umetoa msaada wa Katoni 500 za Taulo za Kike kwa Shule za Sekondari za Wasichana, Mandera iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani na Shule ya Wasichana Manchali iliyoko Chamwino Mkoani Dodoma.
Shule ya Sekondari ya Wasichana, Mandera ambayo ina wanafunzi 584 ilikabidhiwa katoni 250, wakati ile ya Manchali yenye wanafunzi 580 nayo pia ilikabidhiwa katoni 250, zote zikiwa na thamani ya shilingi milioni 16, alisema Afisa Mkuu wa Uhusiano PSSSF Bi. Fatma Elhady kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, wakati akikabidhi katoni 250 za taulo hizo kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mandera, Bi. Regina Abdul Ngereza.

“Msaada huo na mwingine tulioutoa Dodoma ni utekelezaji wa sera yetu ya PSSSF ya Uwekezaji wa kijamii (Corporate Social Investment Policy), na tunaamini taulo hizi zitasaidia kujenga kujiamini kwa wanafunzi hao na hivyo kuondoa uwezekano wa kutohudhuria masomo kwa wasichana wanapokuwa kwenye ada ya kila mwezi.” Alisema Bi. Elhady.
“Taulo hizi zitawasaidia sana wanafunzi wetu na tunashukuru kwa moyo wa upendo kwa kuichagua Shule yetu kwani wenye kuhitaji ni wengi,” alisema Bi Regina Ngereza ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mandera.
Naye Meneja Utawala PSSSF Bi. Fatma Chondo, alikabidhi msaada wa taulo 250 kwa Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Manchali Bw. Severine Msekaa.
” Pamoja na majukumu yetu makuu ya kutoa huduma za hifadhi ya Jamii kwa wanachama wetu, Mfuko pia una jukumu la kurejesha na kuwekeza katika jamii, tunaamini kuwa mafanikio ya taasisi yoyote hayawezi kutenganishwa na ustawi wa Jamii,” alisema.








