Puma Energy Tanzania kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Amend Tanzania, imezindua rasmi awamu ya pili ya kampeni ya ‘Be Road Safe Africa’, mpango wa kimkakati wa usalama barabarani unaolenga kuwawezesha watoto na kuongeza uelewa wa usalama barabarani katika jamii zao.

Awamu hii ya pili inalenga kufikia shule tano za msingi zilizopo maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ambazo ni Kisukuru (Tabata), Kunguru (Goba), Mjimpya (Kurasini), Ufukoni (Kigamboni) na Salasala (Salasala). Kupitia programu hii, watoto wanapewa elimu ya usalama barabarani kwa njia shirikishi na bunifu, ikiwa ni pamoja na shughuli wanazozifurahia kama vile ‘Mahakama ya Watoto’, ambapo watoto wanajifunza kuchukua jukumu la kuwa ‘majaji wa usalama barabarani’ ili kuwawajibisha madereva kwa mienendo yao.
Akiongoza uzinduzi huo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) William Mkonda, alisisitiza dhamira ya serikali kupambana na ajali za barabarani ambazo zimeendelea kugharimu maisha ya maelfu ya Watanzania kila mwaka. “Kampeni hii inakwenda sambamba na juhudi za serikali katika kuhimiza usalama barabarani.
Mwaka 2024 pekee, Tanzania ilishuhudia ajali 1,735 za barabarani ambapo ajali 1,198 zilisababisha vifo vya watu 1,715. Makosa ya kibinadamu kama kupuuzia alama, uzembe wa madereva na mwendokasi vilichangia 97% ya ajali hizo. Tunatoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana nasi katika kuelimisha jamii,” alisema SACP Mkonda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji wa Puma Energy Tanzania, Mhandisi Lameck Hiliyai, alisema: “Usalama ni kiini cha shughuli zetu Puma Energy. Kupitia kampeni hii, tunaendeleza juhudi za kulinda maisha, hasa kwa watoto ambao ni watumiaji wa barabara walioko hatarini zaidi. Tunatekeleza maadili ya HSSE (Afya, Usalama, Ulinzi na Mazingira) kwa vitendo kwa kuwapatia elimu na nyenzo za kuwa salama.”

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa majeraha yatokanayo na ajali za barabarani ni chanzo kikuu cha vifo kwa vijana wa umri wa miaka 10 hadi 19 duniani, na ni sababu ya tatu ya vifo kwa watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 9. Vifo vinavyotokana na ajali za barabarani nchini Tanzania vimefikia kiwango cha 31 kwa kila watu 100,000, ikiwa ni takribani mara 1.7 zaidi ya kiwango cha kimataifa na juu ya wastani wa Afrika. Mbali na vifo na ulemavu, ajali hizi husababisha msongo wa mawazo kwa watoto, kukatisha masomo na changamoto za kiuchumi kwa familia kutokana na gharama za matibabu.
SACP Mkonda aliipongeza Puma Energy Tanzania kwa kuonyesha mfano bora wa uwajibikaji wa kijamii, akisema: “Watoto wa shule zilizo karibu na barabara wako kwenye hatari kubwa ya ajali. Tunashukuru kwa ushirikiano huu na tupo tayari kupanua kampeni hii nchi nzima. Tunatoa wito kwa makampuni mengine kujitokeza kuunga mkono usalama wa barabarani kwa ajili ya ustawi wa jamii wanazozihudumia.”
Awamu ya kwanza ya kampeni hii ilitekelezwa kati ya mwaka 2023 na 2024 katika shule 20 nchini Tanzania, Botswana, Zambia na Zimbabwe, ambapo zaidi ya watoto 38,000 walinufaika na elimu ya usalama barabarani. Awamu ya pili ya kampeni hii inaendelea kutekelezwa mwaka huu katika nchi tano: Tanzania, Botswana, Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini.
Kupitia kampeni ya Be Road Safe Africa, Puma Energy Tanzania na washirika wake wanaendeleza jitihada za kujenga jamii salama, zenye ufahamu mpana kuhusu usalama barabarani kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
