Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ameendelea kudhihirisha utu katika uongozi wake, baada ya kumuasili mtoto mchanga aliyetelekezwa wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora.
Mtoto huyo aliyepewa jina la Grace Samia Suluhu, alitelekezwa mjini Nzega, mkoani Tabora, na amekabidhiwa kwa Rais Dkt. Samia na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai.
Kutokana na hilo, leo Machi 11,2026 Dkt Samia amemuasili Grace katika makazi yake Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Hatua hiyo inadhihirisha utu wa Dkt Samia ambaye anasimamia kile alichokiahidi wakati wa kampeni kupitia kauli mbiu ya ‘Kazi na Utu, Tunasonga Mbele’ ikiwa maana anagusa maisha ya Watanzania kwa kutanguliza utu au ubinadamu mbele.
Akizungumza wakati wa kumkabidhi mtoto huyo, Tukai amesema mtoto huyo aliokotwa Januari 17, 2026 akiwa ametelekezwa eneo jirani na nyumba ya wageni ya Kasulu, Nzega Mjini.
Kwa mujibu Tukai, baada ya kupokea taarifa hizo, alishirikiana na Jeshi la Polisi kumchukua mtoto huyo na kumpeleka hospitalini kwa uchunguzi na uangalizi, huku juhudi za kumtafuta mama yake zikiendelea bila mafanikio.
Hata hivyo, Dkt Samia amemkaribisha mtoto huyo katika familia yake na kuahidi kumpatia malezi, ulinzi na huduma zote muhimu ili akue katika mazingira salama na yenye upendo.
“Wanaotupa watoto hawajui wanalolifanya. Kuliko kumtupa mtoto ni afadhali ukamkabidhi katika mamlaka za kisheria au kituo cha kulelea watoto.
“Kila mtoto aliyezaliwa ni hazina, na hatuijui kesho yake,” amesisitiza Rais Dkt Samia.





