Wananchi wa Korogwe na maeneo mengine ya Tanga wameanza kuona matumaini mapya ya upatikanaji wa maji safi na salama kufuatia utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Kwa miaka kadhaa, licha ya mji wa Korogwe kupitiwa na mto mkubwa na muhimu nchini, mto Pangani, wananchi waliendelea kukumbana na changamoto ya uhaba wa maji safi na salama. Hata hivyo, hali hiyo sasa inaelekea kubadilika kupitia mradi mkubwa wa kuboresha huduma ya maji unaotekelezwa mkoani Tanga Kupitia uwekezaji wa takribani shilingi bilioni 171, serikali imeanzisha mradi unaolenga kuboresha upatikanaji wa maji kwa maelfu ya wananchi wa mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma za msingi karibu zaidi na wananchi.
Mradi huo umebuniwa kuhudumia wilaya nne muhimu za mkoa wa Tanga ambazo ni Wilaya ya Korogwe, Handeni, Muheza pamoja na Wilaya ya Pangani, huku chanzo kikuu cha maji kikiwa ni Mto Pangani.
Ili kuhakikisha maji yanafika kwa uhakika kwa wananchi, kazi kubwa ya ujenzi wa miundombinu imefanyika na inaendelea, ikiwemo ujenzi wa vituo vya kusukuma maji, ulazaji wa bomba kuu la maji lenye urefu wa takribani kilomita 188 pamoja na ujenzi wa matenki makubwa ya kuhifadhia maji ili kuhakikisha maji yanapatikana hata wakati wa mahitaji makubwa.
Lengo la miundombinu hiyo ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa uhakika zaidi kuliko wakati wowote uliopita. Hapo awali uzalishaji wa maji katika eneo hilo ulikuwa takribani lita milioni 5.5 kwa siku, lakini baada ya kukamilika kwa mradi huo uzalishaji unatarajiwa kufikia takribani lita milioni 52 kwa siku, ongezeko la karibu mara tisa ya kiwango cha awali.
Mradi huo unatarajiwa kuhudumia takribani wananchi 868,000 katika wilaya hizo nne, huku hadi sasa utekelezaji wake ukiwa umefikia zaidi ya asilimia 70 na kazi ikiendelea ili kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika kikamilifu na huduma hiyo muhimu ya maji safi na salama.
Kwa mujibu wa taarifa za wataalamu wa sekta ya maji, mradi huo umebuniwa kukidhi mahitaji ya maji kwa zaidi ya miaka 20 ijayo, hatua inayotarajiwa kubadilisha kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi wa mkoa wa Tanga na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo hayo.




