RC Senyamule apongeza utaratibu wa PSSSF kuelimisha wastaafu watarajiwa

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amepongeza utaratibu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kuwajengea uwezo wa namna bora ya maisha nje ya utumishi wa umma kwa wastaafu watarajiwa wanaochangia PSSSF jijini Dodoma Novemba 11, 2024.

Amesema mwelekeo wa serikali ni kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025, eneo mojawapo litakalofanikisha azma hii ni uwekezaji katika viwanda vidogo na vya kati.Kiasi cha mafao kinacholipwa ni kikubwa na iwapo wastaafu wa PSSSF wataelimishwa, fedha hizi zinaweza kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na kuongeza fursa za ajira.         

“Naiona fursa hii katika mpango huu wa PSSSF kwani mafunzo haya yanalenga maeneo ya uwekezaji katika viwanda vidogo vidogo na vya kati, kilimo, biashara na ufugaji, pamoja na soko la fedha, nawaongeza sana.” amesema Senyamule.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Kaimu Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Mbaruku Magawa, amesema,  kwa mwaka 2024/25 pekee Mfuko unatarajia kuwalipa Mafao ya Uzeeni Wastaafu 11,622 jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 560.79, aidha, Mfuko utalipa pensheni ya kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni 980.33 kwa wanufaika wanaotarajiwa kufikia 190,000.

Pia amedokeza kuwa, PSSSF tayari imelipa jumla ya mafao yenye kiasi cha shilingi trilioni 10.46 kwa wanufaika 310,458, tangu kuanzishwa kwake miaka 6 iliyopita.
Kaulimbiu ya semina hiyo ni “Uwekezaji wenye Tija Utakupa Uhakika wa Maisha Baada ya Kustaafu.”

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *