Mhamasishaji Jamii kutoka Shirika la Room to Read katika Kitengo cha Usawa wa Kijinsia, Rogathe Msturo, amesisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kuhamasishwa kuhusu usawa wa kijinsia ili wanawake wapate nafasi, heshima na thamani wanayostahili katika maendeleo ya jamii.
Msturo alitoa wito huo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi mbalimbali pamoja na wakazi wa Temeke na maeneo ya jirani walishiriki katika hafla hiyo ya kijamii.
Alisema maadhimisho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuikumbusha na kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia, akieleza kuwa wanawake wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa katika nyanja zote za maisha.


Aidha, alifafanua kuwa shirika la Room to Read limeamua kushirikiana na Wilaya ya Temeke katika maadhimisho hayo ili kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu haki na nafasi ya mwanamke.
“Kwa kuwa tunafanya kazi na watoto wa kike na wa kiume, tuna jukumu la kuhakikisha tunajenga jamii inayotambua na kuthamini usawa wa kijinsia tangu wakiwa wadogo,” amesema Msturo.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa serikali na wadau mbalimbali kuendelea kuweka msisitizo katika juhudi za kuimarisha usawa wa kijinsia, ili wanawake waweze kupata haki, fursa na thamani sawa katika jamii.






