Klabu ya Coastal Union ipo kwenye mazungumzo ya mwisho na straika wa zamani wa Simba, Adam Salamba, kipa Ali Salim na mshambuliaji chipukizi wa zamani wa Mtibwa Sugar U-20, Athumani Masumbuko ‘Makambo’.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema mazungumzo yanaendelea vizuri na huenda muda wowote wakasajiliwa rasmi, ingawa kuna mambo madogo yanayoshughulikiwa kuhusu Salim.
Salamba aliwahi kucheza Simba mwaka 2018–2019 kabla ya kwenda nje ya nchi, akizichezea JS Saoura ya Algeria na Mehalla El Kubra ya Misri, huku kabla ya hapo akiitumikia Stand United na Lipuli.
Wakati huo huo, Coastal Union imetangaza benchi jipya la ufundi ambapo Kocha Mkuu ni Ali Mohamed Ameir kutoka KVZ Zanzibar, akisaidiwa na Ali Bakari (zamani Uhamiaji).
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Abbas El Sabri alisema wamechagua makocha na wachezaji wenye kiu ya mafanikio na si majina makubwa tu, ili kuleta ushindani na matokeo bora. Coastal ilimaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya nane na pointi 35 baada ya michezo 30.


