Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma(CHAUMMA), Salum Mwalimu ameahidi kutatua tatizo la migogoro ya Wakulima na Wafugaji ndani ya siku 100 akiingia madarakani.
Mwalimu ametoa kauli hiyo leo kwenye mkutanao wa kampeni Kilosa mkoani Morogoro.
Amesema pamoja na migogoro hiyo kuendelea kutesa wananchi lakini wapo baadhi ya watu wanaitumia migogoro hiyo kujinufaisha.

“Hii migogoro ya ardhi ni miradi ya watu, wanaitumia kujinufaisha, inabidi tushughulikie suala hili tulikomeshe, na ndio maana kwenye ilani ya chama chetu tuliliona na tukaiweka, kwamba inabidi ndani ya siku 100 ya serikali ya CHAUMMA tukalitatue.”
Amesema haiwezekani tatizo hilo la Wakulima na Wafugaji badala ya kutatuliwa linazidi kuongezeka.
“Watu hawa wanaoteseka kila siku ni Watanzania na kila siku tunaona viongozi wanakwenda kwao lakini jitihada za kutatua matatizo yao hatuoni, kama siyo miradi ya watu ni nini, CHAUMMA tukiingia madarakani ni lazima tumalize haya,”amesema Mwalimu.




