Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Samia Suluhu Hassan, ametaja miradi ya kitaifa miwili itakayokuza ajira na kuongeza fursa za kibiashara kwa wananchi wa Tabora akiwataka kuzichangamkia ili kukuza uchumi.
Miradi hiyo ni bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) kupitia Tabora hadi Tanga, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Makutopora hadi Isaka (Shinyanga) kupitia Tabora na miundombinu ya barabara.
Ameeleza hayo, leo Ijumaa Septemba 12,2025 wakati akihitimisha kampeni zake za mkoa wa Tabora kabla ya kuelekea mkoani Kigoma kuendelea kusaka kura kupitia mikutano ya hadhara iliyoandaliwa na CCM.
“Mradi wa SGR unapita,Uyui, Nzega na Urambo, katika maeneo hayo kutakuwa na vituo vya watu kushuka na kupanda. Katika maeneo hayo ya vituo kutakuja maendeleo mbalimbali, biashara zitakazowekwa na sekta binafsi.
“Lakini pia maghala ya kuhifadhi bidhaa zitakazofirishwa na reli hii, hizi ni ajira na fursa za biashara ambazo tungewaomba wananchi wa Tabora kuzichangamkia,”amesema Dk.Samia.




