Monday, December 15, 2025
spot_img
HomeBiasharaSBL na NCT wapanua wigo mafunzo ya Learning for Life Arusha

SBL na NCT wapanua wigo mafunzo ya Learning for Life Arusha

Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) wamezindua rasmi awamu ya pili ya programu ya Learning for Life katika Kampasi ya NCT Arusha. Hatua hii ni upanuzi wa ushirikiano ulioanzishwa jijini Dar es Salaam Septemba 2024.

Kupitia awamu hii, zaidi ya vijana 150 watajiunga na mafunzo ya vitendo yanayoendana moja kwa moja na mahitaji ya soko la ajira kwenye hoteli, migahawa na baa katika ukanda wa kaskazini wa utalii.

Awamu hii inafuata mafanikio ya kundi la kwanza jijini Dar es Salaam, ambapo wanafunzi 100 walihitimu mnamo Mei 2025. Ili kuongeza tija na uendelevu, SBL imewekeza kwenye mfumo wa Training-of-Trainers (ToT) kwa wakufunzi wa NCT, utakaowezesha chuo hicho kuendesha mafunzo yajayo kwa uhuru na kutoa vijana walio tayari kwa ajira katika sekta ya utalii na ukarimu – sekta muhimu katika kukuza uchumi wa taifa.

Programu hii inachanganya masomo darasani, mafunzo kwa vitendo na mazoezi ya moja kwa moja kwenye taasisi za sekta. Wanafunzi pia watanufaika na mafunzo kutoka Diageo Bar Academy ikiwemo uendeshaji wa baa, sanaa ya mixology, huduma kwa wateja pamoja na ujuzi muhimu wa maisha kama vile mawasiliano, uongozi na mbinu za kujitangaza.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa NCT, Dk. Florian Mtey alisema:

“Programu hii imefungua milango mipya kwa wanafunzi wetu. Inawaondoa kwenye nadharia pekee na kuwapeleka katika mazingira halisi ya kazi, jambo linaloongeza kujiamini kwao na kuwafanya kuwa tayari kukidhi matarajio ya waajiri. Tunaona fahari kuendeleza ushirikiano huu na SBL hapa Arusha.”

Aidha, NCT imetangaza kuwa kutakuwa na kozi fupi chini ya mpango huu kuanzia Septemba 22 hadi Novemba 2, 2025. Gharama zote za mafunzo zitatolewa na SBL, huku wanafunzi wakigharamia makazi, chakula na usafiri wao binafsi.

Masharti ya Mwombaji:

  • Awe Mtanzania.
  • Awe na barua ya utambulisho kutoka serikali ya mtaa/kijiji au mwajiri.
  • Awe na umri kati ya miaka 15 – 35.
  • Awe na afya njema.
  • Awe na Cheti au sifa ya juu katika Ukarimu au Utalii.

Maombi yanapaswa kuwasilishwa kabla ya Septemba 16, 2025 kupitia tovuti ya chuo: www.nct.ac.tz
au katika kampasi za NCT zilizopo Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.

Mkurugenzi wa Biashara wa Serengeti Breweries Limited, Bw. Christopher Gitau alisema:

“Kwetu SBL tunaamini kuwekeza kwa vijana ni kuwekeza kwenye mustakabali wa jamii. Kupitia Learning for Life, tunawajengea vijana ujuzi wa kiufundi, uongozi, ujasiriamali na uwezo wa kuchangia katika ukuaji wa sekta ya utalii na ukarimu nchini.”

Programu ya Learning for Life ni sehemu ya ajenda ya kijamii ya SBL ijulikanayo kama Spirit of Progress, inayoakisi dhamira ya muda mrefu ya kampuni hiyo katika uwekezaji wa kijamii, ujenzi wa uwezo na kuwawezesha vijana. Kupitia upanuzi huu Arusha, programu hii itazalisha fursa zaidi za ajira na kuimarisha sekta ya utalii na ukarimu nchini Tanzania.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments