Mabingwa watetezi wa CHAN, Senegal, wameweka historia kwa kuwa mabingwa wa pili kushinda mechi yao ya kwanza katika historia ya mashindano hayo baada ya miaka minne.

Senegal iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Nigeria kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, bao likifungwa na Christian Gomis dakika ya 75.
Mara ya mwisho tukio kama hilo lilitokea mwaka 2021, Morocco ilipoishinda Togo 1-0 kwenye CHAN iliyofanyika Cameroon.
Mashindano ya CHAN mwaka huu yanafanyika kwa mara ya nane katika nchi tatu: Tanzania, Kenya na Uganda.
Kwenye mashindano ya mwaka 2023, Morocco, waliokuwa mabingwa watetezi, hawakushiriki kutokana na mzozo wa kisiasa na Algeria waliokuwa wenyeji.
Aidha, historia inaonyesha kuwa mabingwa wa CHAN mara nyingi hushindwa kushinda mechi zao za ufunguzi kwenye fainali zinazofuata, hali inayoifanya Senegal kuwa na mafanikio ya kipekee msimu huu.