Timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, inakutana na Uganda Cubs leo kwenye fainali ya CECAFA U-17, itakayopigwa katika Uwanja wa Hamza Nakivubo, Kampala.

Timu zote tayari zimefuzu kushiriki Fainali za AFCON U-17 zitakazofanyika Machi mwakani nchini Morocco. Serengeti Boys walitinga fainali kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Sudan Kusini, huku Uganda Cubs wakiwafunga Somalia 4-1.
Kocha wa Serengeti Boys, Agrey Morris, amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo muhimu, akiomba sapoti ya Watanzania. Mchezaji Saleh Ally amewahakikishia mashabiki ushindi na kuahidi kurudi na kombe.
Awali, timu hizi zilikuwa Kundi A na mechi yao ilimalizika kwa sare ya bila kufungana. Serengeti Boys wanahitaji kuonyesha nguvu zaidi mbele ya wenyeji Uganda ili kutwaa ubingwa.