SERIKALI imekabidhi vitabu vya elimu ya dini ya sekondari 3,000 kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa lengo la kusambazwa katika shule binafsi zizofundisha somo hilo ambalo kwa mujibu wa waraka wa elimu ya dini ni la lazima kwa ngazi ya msini na sekondari.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam wakati wa makabidhiano ya vitabu hivyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema vitabu hivyo ni sehemu ya nakala 8,000 zilizochapishwa ambako 5,000 zitapelekwa shule za serikali.
Amesema vitabu hivyo viliandaliwa chini ya utaratibu wa chombo maalumu kilichoundwa kwaajili ya kuratibu na kusimamia somo la elimu ya dini ya Kiislamu Tanzania (TISTA) akiahidi kwamba serikali itahakikisha inaendelea kutoa nakala nyingi zaidi ili ziweze kufika kila eneo nchini.
“Kwa dini zote serikali haiwezi kuwa na maamuzi nini kiandikwe, wanaofanya maamuzi ni wale viongozi wa dini wenyewe, haita fika pahali serikali iseme hapana hapa tutafsiri hivi wakati wapo wanazuoni wa Kiislamu, vivyo hivyo kwa upande wa Wakiristo.

“Serikali imeboresha sera ya elimu na mafunzo lakini katika maboresho hayo mafunzo kwa dini zote ni ya lazima kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita, na utekelezaji wake kwa sasa unaenda kwa kuangalia waraka wa elimu namba tano,” amesema Prof. Mkenda.
Amesisitiza kuwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa somo la dini linapaswa kupangiwa vipindi viwili kwa wiki katika shule za msingi na sekondani, pia yatafundishwa na walimu wa madhebebu husika, akieleza kuwa haitaruhusiwa kufundishwa na mwalimu ambaye imani yake ni tofauti na dhehebu husika hata kama kasomea.
