Serikali yapongeza Wiki ya Ubunifu MUHAS, yaahidi kushauri na kusaidia teknolojia za kiafya

DAR ES SALAAM, Aprili 25, 2025 – Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa inaunga mkono jitihada za ubunifu katika sekta ya afya zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), hasa zile zinazolenga kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali za kiafya nchini.

Akizungumza katika hafla ya kufunga Wiki ya Ubunifu ya MUHAS jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Peter Msofe, alisema kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa taasisi za elimu ya juu katika kuibua suluhisho la matatizo ya jamii kupitia teknolojia na bunifu mpya.

“Serikali imeandaa miongozo ya matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence) katika taasisi zake za elimu ya juu. Pia, tunashirikiana na Wizara ya Habari na Mawasiliano kuhakikisha matumizi ya teknolojia hizo yanafuata taratibu sahihi,” alisema Prof. Msofe kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema uamuzi wa kuanzisha Wiki ya Ubunifu umetokana na kuona umuhimu wa kukuza tafiti na teknolojia za kiafya, huku zaidi ya wananchi 300 wakihudumiwa kwa vipimo mbalimbali kama sehemu ya mchango wa chuo kwa jamii.

“Tumeshuhudia ubunifu kwenye vifaa tiba, dawa za asili, vitakasa mikono kama sabuni na pia maboresho ya bidhaa za maji na vidonge. Lengo ni kuhakikisha bunifu hizi zinakuja na njia mbadala, za gharama nafuu lakini zenye tija kwa jamii,” alisema Prof. Kamuhabwa.

Miongoni mwa wabunifu waliopata nafasi ya kuonyesha kazi zao ni Clara Mcharo, mwanafunzi wa mwaka wa nne wa udaktari, ambaye alieleza kuwa mradi wake unalenga kutatua changamoto ya uhaba wa wakunga katika vituo vya afya.

“Katika baadhi ya maeneo, mkunga mmoja anahudumia hadi wagonjwa 1,000. Mfumo wetu unalenga kuwasaidia wakunga hao waweze kuwafuatilia na kuwahudumia wajawazito wengi kwa ufanisi kwa kutumia teknolojia ya kidijitali,” alisema Clara.

Katika wiki hiyo ya ubunifu, wadau mbalimbali wa afya walishirikiana na chuo kutoa huduma za bure za vipimo vya magonjwa yasiyoambukiza kwa wananchi, huku miradi ya bunifu kutoka kwa wanafunzi, watafiti na wataalamu wa afya ikionyeshwa kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kuboresha maisha ya Watanzania.

Wiki ya Ubunifu ya MUHAS, ikiwa ya kwanza kufanyika chuoni hapo, ilianza Aprili 22 na kufikia tamati Aprili 25, 2025.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *